Misri yatangaza tarehe ya uchaguzi wa rais, wagombea 7 kuchuana
(last modified Tue, 26 Sep 2023 13:52:08 GMT )
Sep 26, 2023 13:52 UTC
  • Misri yatangaza tarehe ya uchaguzi wa rais, wagombea 7 kuchuana

Mamlaka ya Kitaifa ya Uchaguzi ya Misri imetengaza kuwa uchaguzi wa rais nchini humo utafanyika mwezi Disemba mwaka huu.

Walid Hamza, Mwenyekiti wa chombo hicho cha kusimamia uchaguzi nchini Misri amesema hayo katika kikao na waandishi wa habari mjini Cairo na kuongeza kuwa, uchaguzi huo utafanyika baina ya Disemba 10 na 12.

"Iwapo uchaguzi utaingia katika duru ya pili, zoezi hilo litafanyika baina ya Januari 8 na 10 2024 ndani ya Misri, na baina ya Januari 5 na 7 nje ya nchi," ameongeza Hamza. Ameeleza bayana kuwa, raia wa Misri walio nje ya nchi watapiga kura baina ya Disemba Mosi na 3.

Ameeleza kuwa, uchaguzi wa rais utakuwa chini ya uangalizi kamili wa Idara ya Mahakama ya Misri. Mwenyekiti wa Mamlaka ya Kitaifa ya Uchaguzi ya Misri amebainisha kuwa, wenye azma ya kugombea kiti hicho watapewa fursa ya kuwasilisha maombi na nyaraka zao kwa tume hiyo baina ya Oktoba 5 na 14. 

Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri ambaye serikali yake imekuwa ikikabiliwa na maandamano ya kulalamikia hali ya kiuchumi na kisiasa ya nchi hiyo, anatazamia kugombea muhula wa tatu, ingawaje mpaka sasa hajatangaza rasmi azma yake hiyo.

Rais Abdel Fattah al-Sisi wa Misri

Wananchi wa Misri wanamtuhumu Sisi ambaye muhula wake wa pili wa miaka 6 unamalizika mwaka ujao 2024, kwamba ameshindwa kukabiliana na mfumuko wa bei uliokithiri, kupanda kwa bei za bidhaa na kuadimika bidhaa za msingi, mbali na kushuka thamani ya sarafu ya pauni.

Mbali na Sisi, kuna shakhsia wengine saba wa kisiasa wanaotazamiwa kuchuana kwenye uchaguzi wa rais, akiwemo Ahmed Tantawi, mbunge wa zamani ambaye anatazamiwa kutoa ushindani mkali dhidi ya Sisi.