27 wafariki, 100 hawajulikani waliko baada ya mashua kupinduka kaskazini ya Nigeria
(last modified Sat, 30 Nov 2024 07:08:56 GMT )
Nov 30, 2024 07:08 UTC
  • 27 wafariki, 100 hawajulikani waliko baada ya mashua kupinduka kaskazini ya Nigeria

Watu wasiopungua 27 wamefariki dunia na zaidi ya 100 hawajulikani walipo baada ya mashua kupinduka kaskazini mwa Nigeria.

Msemaji wa shirika la usimamizi wa matukio ya dharura katika jimbo la Niger, Ibrahim Audu, ameviambia vyombo vya habari kuwa abiria wapatao 200 walikuwemo kwenye mashua iliyokuwa ikitoka jimbo la Kogi kuelekea jimbo jirani la Niger, wakati mashua hiyo ilipopinduka kwenye Mto Niger jana asubuhi.
 
Sandra Musa, msemaji wa huduma za dharura katika jimbo la Kogi amesema, waokoaji walifanikiwa kuopoa miili 27 kutoka mtoni humo kufikia Ijumaa jioni huku wazamiaji wa eneo hilo wakiendelea kutafuta miili mingine.
 
Musa ameongeza kuwa, hakukuwa na mtu aliyenusurika aliyepatikana takribani saa 12 baada ya tukio hilo kutokea. Mashua hiyo ilikuwa ikiwasafirisha abiria hao ambao wengi wao walikuwa wanawake kuelekea kwenye soko la chakula.
 
Mamlaka husika haijathibitisha chanzo cha kuzama mashua hiyo lakini vyombo vya habari vya ndani vimedokeza kuwa huenda mashua hiyo ilikuwa imejaa kupita kiasi. Msongamano wa watu kwenye mashua ni jambo la kawaida katika sehemu za mbali za Nigeria ambapo ukosefu wa barabara nzuri huwaacha watu wengi bila ya kuwa na njia mbadala za usafiri.
 
Matukio hayo mabaya ya ajali yanazidi kuwa chanzo cha wasiwasi nchini Nigeria, nchi yenye watu wengi zaidi barani Afrika, huku mamlaka zikijitahidi kutekeleza hatua za usalama na kanuni za usafiri wa majini.../