Usalama waimarishwa Somalia baada ya makumi ya watu kuuawa Lafole
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i10318-usalama_waimarishwa_somalia_baada_ya_makumi_ya_watu_kuuawa_lafole
Hatua kali za kiusalama zimechukuliwa nchini Somalia baada ya mlipuko wa bomu uliotokea kandokando ya barabara katika mji wa Lafolena kuua makumi ya watu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jun 30, 2016 10:32 UTC
  • Usalama waimarishwa Somalia baada ya  makumi ya watu kuuawa Lafole

Hatua kali za kiusalama zimechukuliwa nchini Somalia baada ya mlipuko wa bomu uliotokea kandokando ya barabara katika mji wa Lafolena kuua makumi ya watu.

Afisa mwandamizi wa polisi ya Mogadishu Abidkadir Mohamed amesema kuwa, usalama umeimarishwa katika barabara za Mogadishu na kwamba maafisa wa serikali walikuwa tayari wametahadharisdha kuhusu vitisho vilivyotolewa na kundi la kigaidi la al Shabab.

Watu wasiopungua 20 wameripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulizi la bomu mapema leo katika mji wa Lafole, kusini magharibi mwa Somalia. Inasadikiwa kuwa abiria wote wa basi hilo dogo lililokuwa njiani katika barabara ya Mogadishu Afgoye, wameuawa.

Hadi sasa hakuna mtu au kundi lililotangaza kuhusika na hujuma hiyo japokuwa kundi la kigaidi la al Shabab linaelekezewa kidole cha tuhuma kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara yanayofanywa na wanachama wake dhidi ya raia na maeneo ya umma nchini Somalia. Hayo yanajiri katika hali ambayo, Jumamosi iliyopita, watu 17 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulizi la kigaidi la wanachama wa ash-Shabaab dhidi ya hoteli ya Nasa Hablod iliyoko katika mji mkuu Mogadishu.