Oct 25, 2023 07:36 UTC
  • Muswada wa kujinaisha uhusiano na Israel wavuka kiunzi cha kwanza Tunisia

Kamati ya Bunge la Tunisia imepasisha katika marhala ya kwanza muswada wa sheria inayotaka vitendo vya kuanzishwa uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel kuwa kosa la jinai.

Kamati ya Haki na Uhuru ya Bunge la Tunisia iliudhinisha muswada wa sheria hiyo jana Jumanne, wakati huu ambapo wananchi wa nchi hiyo ya Kiarabu ya kaskazini mwa Afrika wanaendelea kuandamana kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wa Ukanda wa Gaza.

Baada ya kupasishwa na kamati hiyo, sasa muswada huo utawasilishwa Bungeni kwa ajili ya kujadiliwa na pia kufanyika kikao cha kupokea maoni ya wananchi juu ya muswada huo kabla ya kupigiwa kura.

Hela Jaballah, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhuru ya Bunge la Tunisia amesema, "Muswada wa sheria hii una vipengele 7, ambapo adhabu yake ni kufungo cha maisha jela."

Amebainisha kuwa, kufanya uhusiano wa kawaida, mawasiliano ya kibiashara, shughuli za kijamii au kuwa na uhusiano wa kijeshi na kiintelijensia na Israel kutakabiliwa na adhabu kali.

Wananchi wa Tunisia wamekuwa wamekuwa wakifanya maandamano ya kulaani dhulma na mauaji ya wananchi madhulumu wa Palestina yanayofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel kila leo.

Watunisia katika maandamano wa kuonyesha mshikamano wa Wapalestina

Agosti mwaka huu pia, Rais Kais Saied wa Tunisia alikanusha vikali madai kuwa taifa hilo lina azma ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel. Akizungumza na mabalozi wapya walioteuliwa kuiwakilisha Tunisia katika nchi za Kiarabu na zisizo za Kiarabu, Rais Kais Saied alisema: Kwa wanaozungumzia (kuanzishwa) uhusiano wa kawaida (na Israel), nawaleza kuwa msamiati huo hauna maana yoyote katika kamusi yangu."

Alisema kadhia ya Palestina ina umuhimu mkubwa kwa taifa hilo na kusisitiza kwamba, kuna haja ya milki za Palestina kurejeshwa kwa wananchi wa Palestina.

Tags