Rais Nkurunziza: Tunajitahidi kuimarisha usalama na amani Burundi
Rais Pirre Nkurunziza wa Burundi amesema kuwa, serikali yake imezimia kuimarisha usalama na amani nchini humo.
Sanjari na kusisitizia suala hilo, Rais Nkurunziza ameongeza kuwa, serikali itakabiliana na aina yoyote ya uvunjaji wa amani nchini Burundi. Amesema kuwa hivi sasa Burundi inakabiliwa na changamoto nyingi, kubwa zaidi ikiwa ni changamoto ya usalama na amani, lakini akasisitiza kuwa, serikali inakabiliana na maadui kwa irada thabiti. Rais wa Burundi aliyeyasema hayo hapo jana kwa mnasaba wa siku ya uhuru wa nchi hiyo alisisitiza kuwa, uhuru wa taifa hilo uliofikiwa kwa juhudi kubwa za watu waliotangulia, haufai kuvurugwa kirahisi na baadhi ya pande za ndani na nje ya nchi hiyo. Rais Pirre Nkurunziza ameyasema hayo katika hali ambayo, hatua yake ya kutaka kuendelea kusalia madarakani hapo mwezi Aprili mwaka jana, ndio iliitumbukiza nchi hiyo katika mgogoro wa kisiasa na kusababisha mamia ya watu kuuawa na maelfu ya wengine kuwa wakimbizi.