Kiongozi wa upinzani ashinda uchaguzi wa rais Liberia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i104912
Kinara wa upinzani nchini Liberia, Joseph Boakai ameibuka mshindi kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa rais, na kumbwaga Rais anayeondoka, George Weah aliyekuwa anagombea muhula wa pili.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Nov 18, 2023 05:40 UTC
  • Kiongozi wa upinzani ashinda uchaguzi wa rais Liberia

Kinara wa upinzani nchini Liberia, Joseph Boakai ameibuka mshindi kwenye duru ya pili ya uchaguzi wa rais, na kumbwaga Rais anayeondoka, George Weah aliyekuwa anagombea muhula wa pili.

Kwa mujibu wa matokeo ya asilimia 99.5 ya kura zilizohesabiwa mpaka sasa na kutangazwa na Kamisheni ya Uchaguzi ya Liberia, Boakai ameshinda kwa kupata karibu asilimia 51 ya kura, huku Weah akipata asilimia 49.

Wananchi wa Liberia walipiga kura Jumanne iliyopita katika duru ya pili ya uchaguzi huo uliowachuanisha Rais George Weah na Makamu wa Rais wa zamani Joseph Boakai baada ya mchuano mkali wa duru ya kwanza, ambapo hakuna aliyeweza kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura.

George Weah, 57, aliongoza kwenye duru ya kwanza ya uchaguzi huo mwezi Oktoba, kwa kupata asilimia 43.83 ya kura, na Boakai alipata asilimia 43.44.

Boakai (kulia) na George Weah

Boakai, 78, ni mwanasiasa mkongwe ambaye kuanzia mwaka 2006 hadi 2018 alikuwa naibu wa Ellen Johnson Sirleaf, rais wa kwanza mwanamke barani Afrika kwa kuchachaguliwa kidemokrasia.

Katika uchaguzi wa mwaka 2017, George Weah ambaye ni mchezaji soka mashuhuri wa zamani alishinda kwa zaidi ya asilimia 61 ya kura.

Tayari Weah amempongeza Boakai kwa ushindi huo. Katika hotuba yake kupitia radio ya taifa, Weah amesema, "Chama cha CDC kimepoteza uchaguzi, lakini Liberia imeibuka mshindi. Huu ni wakati wa kutanguliza mbele maslahi ya taifa, badala ya maslahi binafsi."