Azma ya serikali ya Burundi kwa ajili ya kurejesha usalama nchini humo
-
Rais Pierre Nkurunziza wa Burundi
Rais wa Burundi ametangaza azma ya serikali yake ya kutatua masuala kadhaa, ikiwemo kurejeshwa usalama nchini humo.
Akiashiria kuwepo uvunjifu wa amani nchini Burundi, Rais Pierre Nkurunziza amesema kuwa, hii leo taifa hilo linakabiliwa na vizingiti vingi kwa ajili ya kurejesha usalama na utulivu nchini humo, lakini akasisitiza kuwa serikali itakabiliana vilivyo na maadui wanaoharibu usalama wa nchi hiyo. Raia Nkurunziza amesisitiza kuwa, uhuru wa taifa hilo uliofikiwa kwa juhudi kubwa za watu waliotangulia, haufai kuvurugwa kirahisi na baadhi ya pande za ndani na nje ya nchi hiyo. Kadhalika amesema kuwa, mtu yeyote ambaye hataki kwenda mwelekeo sawa na matakwa ya wananchi, basi atakabiliwa na nguvu za sheria. Siku chache kabla ya sherehe za miaka 54 ya uhuru wa nchi hiyo, rais huyo alitoa ujumbe kwa wananchi wa Burundi akiwataka kushirikiana na serikali katika kukabiliana na changamoto tofauti za kiuchumi na kijamii. Rais Pierre Nkurunziza alikosoa mwenendo wa wapinzani wa serikali yake akisema kuwa, malalamiko yao ndio chanzo cha ukosefu wa usalama nchini Burundi. Matamshi ya rais huyo yanajiri katika hali ambayo, mgogoro wa kisiasa wa zaidi ya mwaka mmoja sasa, uliibuka kufuatia azma yake ya kutaka kubakia madarakani kwa muhula wa tatu mfululizo, mgogoro ambao umezidi kupanuka siku hadi siku. Hali hiyo imeifanya dhada ya uwezekano wa kuibuka vita vya ndani nchini Burundi, kuwa na nguvu. Wapinzani wanamtuhumu Rais Nkurunziza kuwa, hatua yake ya kubakia madarakani, ni kinyume cha sheria na kwa msingi huo wamesisitiza kuendeleza mapambano hadi pale watakapomuondoa madarakani. Hii ni katika hali ambayo, chama tawala cha CNDD-FDD kinasisitiza kuwa, kusalia madarakani rais huyo kumeenda sambamba na katiba. Ni kwa muda sasa Burundi imegeuka kuwa ulingo wa mivutano ya kisiasa. Kwa mujibu wa weledi wa mambo, kuwepo silaha mikononi mwa makundi ya wapinzani wa kisiasa kumechangia pakubwa kuongezeka mgogoro wa nchi hiyo mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC. Kuongezeka mauaji ya kisiasa ya kuvizia kwa upande mmoja, na upande mwingine kamatakamata na mauaji dhidi ya wapinzani vinavyofanywa na maafisa usalama wa serikali, kumeifanya hali ya mambo kuwa mbaya zaidi nchini Burundi. Kwa mujibu wa ripoti ya Umoja wa Mataifa na taasisi za kutetea haki za binaadamu nchini humo, zaidi ya watu 400 wameuawa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja pekee uliopita. Wakati huo huo, ripoti za mashirika ya haki za binaadamu, zimeelezea kuwepo ukandamizaji mkubwa wa haki za binaadamu na vitendo vya utumiaji mabavu nchini humo. Hali ya kisiasa na machafuko yanayoshuhudiwa nchini Burundi vimewafanya weledi wa mambo kutabiri uwezekano wa kushadidi matatizo ya kiuchumi nchini Burundi. Kwa mujibu wa weledi hao hivi sasa kiwango cha uzalishaji nchini kimepungua sana ikilinganishwa na miaka iliyopita. Mbali na hayo, Burundi pia inakabiliwa na ufisadi wa fedha, ongezeko la kiwango cha ukosefu wa ajira, kuongezeka gharama za maisha kwa raia wa kawaida suala ambalo limeyafanya maisha ya Warundi wengi kuwa magumu. Matatizo hayo yanashuhudiwa nchini humo katika hali ambayo mafuriko yaliyotokea hivi karibuni, yameshadidisha ugumu wa maisha kwa wananchi wa Burundi. Hivi sasa matamshi ya Rais Pierre Nkurunziza yanaweza kutathminiwa kuwa ni hatua moja kwa ajili ya kujaribu kutuliza hali ya mambo na kuwaita wananchi kwenye kudumisha amani na maridhiano ya kitaifa. Viongozi wa Umoja wa Kiafrika wamesisitiza kuwa hawako tayari kushuhudia vita vita vingine katika eneo. Hii ni katika hali ambayo weledi wa mambo wanaamini kuwa, mgogoro wa nchi hiyo utatatuliwa tu kwa pande hasimu kuketi kwenye meza ya mazungumzo na kufikia mwafaka wa kisiasa utakayoyashirikisha makundi yote.