Dec 02, 2023 05:59 UTC
  • UN yaiondoea vikwazo vya silaha Somalia, yahitimisha shughuli zake za kisiasa nchini Sudan

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio la kuondoa vikwazo vya mwisho vya silaha dhidi ya serikali ya Somalia na vikosi vyake vya usalama, huku likihitimisha pia shughuli za ujumbe wake wa kisiasa katika nchi ya Sudan iliyokumbwa na vita.

Baraza hilo lenye wanachama 15 limepitisha maazimio mawili yaliyoandaliwa na kuwasilishwa na Uingereza: moja likiwa ni la kuondoa vikwazo kamili vya silaha kwa Somalia na lingine la kuweka tena vikwazo vya silaha kwa kundi la kigaidi la al Shabaab lenye mafungamano na mtandao wa al Qaeda.
 
Azimio la kuondoa vikwazo vya silaha linaeleza kuwa linatekelezwa "kwa ajili ya kuepuka shaka, kwamba hakuna vikwazo vya silaha itakavyowekewa Serikali ya Shirikisho la Jamhuri ya Somalia."
 
Akizungumzia uamuzi huo wa Baraza la Usalama, Balozi wa Somalia katika Umoja wa Mataifa Abukar Dahir Osman amesema, kuondolewa vikwazo vya silaha vitaiwezesha serikali ya nchi hiyo kukabiliana na vitisho vya usalama.
Aidha, Osman ameeleza kwamba, uamuzi huo unawapa ruhusa pia ya kuimarisha uwezo wa vikosi vya usalama kwa kupata silaha kubwakubwa na vifaa muhimu ili kulinda ipasavyo raia wa Somalia na taifa lao.
Wanamgambo wa Al Shabaab

Katika hatua nyingine na kwa ombi la mamlaka za Sudan, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa jana hiyohiyo lilihitimisha shughuli za ujumbe wake wa kisiasa katika nchi ya Afrika iliyokumbwa na mapigano ya zaidi ya miezi saba sasa kati ya vikosi vitiifu kwa majenerali wawili hasimu wa Jeshi na wa Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF).

Kufuatia barua iliyotumwa na Khartoum kutaka kusitishwa mara moja shughuli za Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Usaidizi wa Mpito nchini Sudan [UNITAMS], Baraza la Usalama limepitisha azimio la kusitisha rasmi majukumu yake hadi kufikia Jumapili.

UNITAMS ilitumwa nchini Sudan mnamo mwaka 2020 kusaidia na kuunga mkono mabadiliko ya kidemokrasia nchini humo kufuatia kuanguka mwaka mmoja kabla yake utawala wa kiongozi mkongwe Omar al Bashir, ambaye alikabiliwa na mashinikizo ya jeshi na maandamano makubwa ya umma.../

Tags