Miripuko kusini mwa Nigeria
Kundi linalojulikana kwa jina la "Walipizaji kisasi wa Niger Delta" limekiri kuhusika na miripuko mitano mikubwa katika taasisi za mafuta na gesi katika eneo la Niger Delta kusini mashariki mwa Nigeria.
Kundii hilo la uasi limedai kuwa miripuko imetokea katika mabomba ya Shirika la Taifa la Mafuta la Nigeria ambayo yanaungana na kiwanda cha kusafishia mafuta cha Warri na katika mabomba mengine mawili ya mafuta yanayomilikiwa na Shirika la Mafuta la Taifa na Shirika la Mafuta la Chevron. Kundi hilo la " Walipizaji Kisasi wa Niger Delta" limekuwa likitekeleza mashambulizi mengi katika visima vya mafuta na gesi huko kusini mwa Nigeria tangu kuanza mwaka huu wa 2016.
Kundi hilo la wanamgambo linataka kupatiwa mgawo wa mapato yanayotokana na uuzaji mafuta ya eneo tajiri kwa mafuta la Niger Delta. Wakazi wa Niger Delta wanaishi katika hali ya umaskini licha ya eneo hilo kuwa na utajiri mkubwa wa mafuta. Kundi hilo pia kama yalivyo makundi mengine ya wanamgambo, linapigania kuwa huru na kujitawala kisiasa eneo la Niger Delta mbali na kutaka kupatiwa mgawo sawa wa pato la mafuta yanayouzwa katika eneo hilo. Wakati huo huo Gavana wa Benki Kuu ya Nigeria ametahadharisha kuhusu athari hasi za uharibifu unaofanywa katika sekta ya mafuta na gesi kwa uchumi wa nchi hiyo. Kushadidi mashambulizi ya uharibifu katika taasisi na visima vya mafuta huko Nigeria, hadi sasa kumesababisha kupungua uzalishaji mafuta wa nchi hiyo na kufikia mapipa milioni moja na laki sita kwa siku.
Hii ni katika hali ambayo katika bajeti ya Nigeria ya mwaka huu uzalishaji mafuta wa nchi hiyo umetabiriwa kufikia mapipa milioni mbili na laki mbili. Wakati huo huo kupungua bei ya mafuta katika soko la kimataifa pia kumetoa pigo jingine kwa uchumi na mapato ya serikali ya Nigeria.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria mwezi Juni mwaka huu alisisitiza kwamba wanamgambo wanaoripua mabomba ya mafuta huko kusini mwa nchi watakabiliwa vikali; na kwamba taasisi na viwanda vya kusafisha mafuta pia vitakarabatiwa. Weledi wa mambo wanaamini kuwa miripuko mtawalia katika eneo lenye utajiri wa mafuta na gesi huko kusini mashariki mwa Nigeria inaonyesha namna kundi hilo la Walipizaji Kisasi wa Niger Delta linavyotekeleza mashambulizi yake kwa ujasiri mkubwa. Kundi hilo limetahadharisha kuwa kufanyiwa ukarabati na kujenga upya mabomba ya mafuta huko Niger Delta itakuwa ni kazi bure madhali serikali ya Nigeria imeshindwa kulitimizia matakwa yake. Kundi la uasi la Wanamgambo Walipizaji Kisasi wa Niger Delta japokuwa ni kundi jipya, lakini vitendo vyake kama vile hujuma dhidi ya mabomba ya kusafirishia mafuta na hasara linazoyasababisha mashirika ya mafuta ya nchi za Magharibi kama lile la Chevron, vina rekodi ya muda mrefu. Kwa mtazamo huu, kundi hilo linatumia vitendo vyake vya uharibifu, miripuko na kuwateka nyara wafanyakazi wa nchi za nje kama wenzo wa kufikia malengo yake.
Wakazi wa eneo la Niger Delta wanafikia karibu milioni 31 huku kukiwa na makabila 40 katika eneo hilo. Jamii ya watu wa Ogoni na Ijaw wanahesabiwa kuwa miongoni mwa waasi wa Harakati ya Wananchi kwa ajili ya kupigania haki za raia maskini wa kusini mashariki mwa Nigeria. Ken Sarowiwa alikuwa mmoja wa viongozi wa Harakati ya Kabila la Ogoni ambaye alinyongwa mwaka 1998 wakati wa utawala wa Sani Abacha dikteta wa kijeshi wa wakati huo wa Nigeria. Mwezi Septemba mwaka 2008 harakati nyingine ilianzisha vita vya kuwania mafuta dhidi ya serikali ya Nigeria, hata hivyo waasi wengi waliweka chini silaha zao kufuatia msamaha uliotolewa na serikali mwaka 2009.
Kundi la Uasi la Walipizaji Kisasi wa Niger Delta limejitokeza na kudai kuwa linataka kuhuisha haki zilizopotea za raia maskini wa eneo hilo. Kwa kuzingatia miripuko mikubwa iliyolikumba eneo la Niger Delta tangu mwanzoni mwa mwaka huu; kinara wa kundi hilo amesema kundi hilo limeazimia kuendeleza mashambulizi yake madhali serikali ya Nigeria imeshindwa kukubali matwaka yake. Weledi wa mambo wanaamini kuwa serikali ya Nigeria inapasa kuweka katika ajenda yake ya kazi mapato yanayotokana na uuzaji wa mafuta ghafi na suala la uboreshaji wa hali ya maisha ya raia maskini wa eneo la Niger Delta. Ahadi tupu zinazotolewa na rais wa nchi ambazo zimewahi kukaririwa huko nyuma, kamwe haziwezi kuwaridhisha wanamgambo hao wala kuwa suluhisho la matatizo ya ukosefu wa ajira na umaskini miongoni mwa vijana wa eneo tajiri kwa mafuta la Niger Delta.