Dec 11, 2023 11:55 UTC
  • ECOWAS yatambua rasmi Baraza la Kijeshi la Niger

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) imelitambua rasmi kwa njia isiyo ya moja kwa moja Baraza la Kijeshi linalotawala Niger.

Katika mkutano wao uliofanyika katika mji wa Nigeria, Abuja, viongozi wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, (ECOWAS) wamepitisha misimamo inayoonyesha kwamba kundi hilo limetambua kwa muda Baraza la Kijeshi linalotawala Niger na kufuta tishio lake la hapo awali la kuishambulia nchi hiyo kijeshi iwapo Mohammed Bazoum, rais aliyeondolewa madarakani wa Niger, katika mapinduzi ya Julai 2023, hatarejeshwa madarakani.

Dr. Omar Alieu Touray, mkuu wa Tume ya ECOWAS, ametangaza katika mkutano wa jumuiya hiyo kwamba timu ya wakuu wa nchi wanachama wa ECOWAS inajadiliana na jeshi linaloongoza Niger juu ya mpango wa muda mfupi wa kukabidhi madaraka

Hapo awali, wakuu wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi walikata uhusiano wao na Niger baada ya jeshi kuchukua madaraka kwa kumpindua Muhammad Bazoum.

Baada ya kuchukua madaraka ya nchi, wanajeshi waliofanya mapinduzi walitoa wito wa kufukuzwa vikosi vya wanajeshi wa kigeni, haswa Ufaransa kutoka Niger na kukomesha uingiliaji wa Paris katika masuala ya ndani ya nchi hiyo. 

Tags