Dec 20, 2023 03:04 UTC
  • AU yataka pande hasimu Sudan zisitishe mapigano

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ametoa mwito kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) na Jeshi la Sudan kusitisha uhasama na mapigano mara moja, na kwenda kwenye meza ya mazungumzo kwa shabaha ya kurejesha utulivu, uthabiti na amani endelevu katika nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika.

Moussa Faki Mahamat amesisitiza kuwa, AU ipo tayari kusimamia mazungumzo ya kuupatia ufumbuzi mzozo baina ya pande mbili hasimu za Sudan.

Mahamat ameeleza katika taarifa kuwa, Umoja wa Afrika unatiwa wasi wasi na taarifa za kupanuka mgogoro nchini Sudan.

Taarifa ya AU imekuja siku chache baada ya vyombo vya habari kuripoti kuwa, Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) vinapigana na Jeshi la Sudan nje ya mji wa Wad Madani katika Jimbo la Al-Jazira (katikati mwa Sudan), na kwamba mapigano hayo yamelazimisha maelfu ya raia kukimbia makazi yao na kuelekea maeneo salama.

Mji huo ulikuwa umepokea mamilioni ya watu walioukimbia mji mkuu Khartoum, baada ya kuibuka mapigano nchini humo mwezi Aprili mwaka huu.

Mapigano Sudan

Juhudi za upatanishi wa kuhitimisha mapigano ya wenyewe kwa wenye nchini Sudan zimeambulia patupu hadi sasa, huku kila mmoja kati ya wababe wa vita hivyo, Abdel Fattah Al-Burhan na Jenerali muasi, Mohamed Hamdan Dagalo (Hemedti), akiendelea kung'ang'ania misimamo yake.

Siku chache zilizopita, Al-Burhan alitangaza kwamba hatakuwa tayari kukutana na Jenerali muasi, Mohamed Hamdan Dagalo ila baada ya kukubali usitishaji vita wa kudumu nchini humo, na kuondoka kwa Vikosi vya Msaada wa Haraka (RSF) mjini Khartoum.

Watu zaidi ya 12,000 wameuawa katika mapigano baina ya pande mbili hizo, wengine 33,000 wamejeruhiwa huku wengine zaidi ya milioni 7 wakilazimika kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi hiyo.

Tags