Tahadhari ya Umoja wa Afrika kwa wanamgambo wa al-Shabab
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1075-tahadhari_ya_umoja_wa_afrika_kwa_wanamgambo_wa_al_shabab
Mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika nchini Somalia ametahadharisha kuhusiana na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabab.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 12, 2016 04:36 UTC
  • Tahadhari ya Umoja wa Afrika kwa wanamgambo wa al-Shabab

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Afrika nchini Somalia ametahadharisha kuhusiana na harakati za kundi la kigaidi la al-Shabab.

Francisco Madeira ametoa indhari hiyo katika mkutano na waandishi wa habari mjini Mogadishu Somalia na kutangaza kuwa, wanachama wa al-Shabab wana mpango wa kuvichafulia jina vikosi vya kusimamia amani vya Umoja wa Afrika nchini humo AMISOM. Ripoti zinaonesha kuwa, wapiganaji wa kundi la kigaidi la al-Shabab la Somalia wanapanga kufanya wimbi la mashambulizi nchini Somalia wakiwa wamevalia magwanda ya kijeshi ya kikosi cha askari wa kulinda amani wa Umoja wa Afrika nchini humo, AMISOM. Ripoti za kiintelijensia zinaonesha kuwa, wanamgambo wa al-Shabaab wanapanga kutekeleza hujuma za kigaidi nchini Somalia wakitumia sare za kijeshi walizochukua baada ya kushambulia kambi tofauti za AMISOM. Huko nyuma, kufuatia muungano wa kikanda dhidi ya al-Shabab, miji kadhaa na bandari muhimu kama ya Kismayo zilikombolewa toka mikononi mwa wanamgambo hao. Hii ni katika hali ambayo, hadi mwaka 2010 zaidi ya nusu ya ardhi ya Somalia ilikuwa ikidhibitiwa na wanamgambo hao wenye mfungamano na mtandao wa al-Qaeda. Tarehe 14 mwezi uliopita wa Januari, kundi la al-Shabab lilifanya shambulio kubwa dhidi ya wanajeshi wa Kenya walioko chini ya mwavuli wa kikosi cha kusimamia amani huko Somalia na kuwaua mia moja kati yao. Hujuma hiyo ya al-Shabab ilionesha kuwa, kundi hilo lingali tisho. Aidha kabla ya hapo kundi la kigaidi la al-Shabab lilishambulia hoteli na mkahawa wa ufukweni katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, ambapo watu wanaokadiriwa kufikia 20 waliuawa.

Wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, mkakati na stratejia ya sasa ya viongozi wa al-Shabab ni kushadidisha hujuma na mashambulio yao nchini Somalia na katika nchi za eneo. Inaonekana kuwa, kundi hilo likitumia hadaa linataka kwa namna fulani kufidia nafasi yake liliyoipoteza kutokana na kukombolewa maeneo mengi liliyokuwa likiyadhibiti.

Kwa hakika makundi mithili ya al-Shabab wakati mwingine yakiwa na lengo la kufidia udhaifu wao hufanya hima ya kuzihadaa fikra za waliowengi kwa maslahi yake. Aidha wakati mwingine magaidi hushadidisha mashambulio dhidi ya raia ili kuzitia katika mashinikizo nchi husika na hivyo kuzifanya zisichukue hatua za kijeshi dhidi yao. Kwa sasa makamanda wa kikosi cha kusimamia amani cha Umoja wa Afrika nchini Somalia AMISOM sanjari na kusisitiza juu ya kuwa macho na harakati za wenye kufurutu ada, wamewataka wananchi kutoa taarifa kwa viongozi wa sehemu zao pindi wanaposhuhudia nyendo za kutia shaka na zisizo za kawaida.