Jan 29, 2024 03:03 UTC
  • Mali, Burkina Faso na Niger zajiondoa kwenye jumuiya ya ECOWAS

Tawala za kijeshi katika nchi za Mali, Burkina Faso na Niger zimetangaza kuyaondoa 'mara moja' mataifa kwenye Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS).

Viongozi wa serikali za kijeshi za nchi hizo za eneo la Sahel huko magharibi mwa Afrika walitangaza hayo jana Jumapili na kuutaja uamuzi huo kuwa huru na wenye kutia nguvu mamlaka ya kujitawala mataifa hayo.

Nchi hizo tatu ambazo ni makoloni ya zamani ya Ufaransa na ambazo zimekuwa zikiendeshwa na tawala za kijeshi tangu 2020, zimekuwa kwenye msuguano na uongozi wa ECOWAS kwa muda mrefu sasa.

Nchi hizo tatu za magharibi mwa Afrika huko nyuma zilisimamishiwa uanachama wa ECOWAS, huku Mali na Niger zikiwekewa vikwazo vikali na jumuiya hiyo ya kieneo.

Wanajeshi walichukua hatamu za ungozi nchini Niger Julai mwaka jana kufuatia mapinduzi ya kijeshi, huku mapinduzi kama hayo yakifanyika Burkina Faso mwaka 2022 na Mali mwaka 2020.

Septemba mwaka jana, Mali, Burkina Faso na Niger zilisaini mkataba wa ulinzi wa pande tatu, unaozifunga nchi hizo tatu za Sahel kusaidiana iwapo kutatokea shambulio la kijeshi dhidi ya yeyote kati yao.

Mkataba huo wa pamoja wa usalama wa nchi hizo tatu za Afrika Magharibi ulipewa jina la " Muungano wa Nchi za Sahel."

 

Tags