Jan 30, 2024 07:22 UTC
  • Kujiondoa Mali, Niger na Burkina Faso kwenye Jumuia ya ECOWAS

Nchi tatu za Niger, Burkina Faso na Mali zimetangaza kujiondoa kwenye Jumuia ya Kiuchumi ya Magharibi mwa Afrika ECOWAS kutokana na kutokuwa na imani na siasa na sera za jumuia hiyo.

Katika taarifa yao ya pamoja, Ibrahim Traore, Kanali Assimi Goita na Jenerali Abdur Rahman Tiani, viongozi wa Burkina Faso, Mali na Niger kwa mpangilio, wamesema kuwa, Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) ni shirika linalodhibitiwa na  madola za kigeni na hivyo wameamua kutangaza uamuzi wao wa pamoja wa kujiondoa katika shirika hilo.

Niger, Mali na Burkina Faso ni nchi tatu zenye umuhimu mkubwa katika eneo la Magharibi mwa Afrika ambazo katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni zimeshuhudia matukio makubwa ya kisiasa kwa kadiri kwamba na hivi sasa  nchi hizo zinatawaliwa na serikali zilizo dhidi ya ukoloni wa Ufaransa na madola ya kibeberu. Viongozi wa kijeshi wa nchi hizo wanaungwa mkono na wananchi kutokana na kufanikiwa kwao kuwatimua askari wa madola ya kibeberu ya Magharibi kama vile Ufaransa kwenye nchi hizo.

Kwa hakika nchi hizo tatu za Niger, Mali na Burkina Faso ambazo zina rasilimali nyingi katika eneo la Afrika Magharibi, zimekuwa zikipewa umuhimu maalumu  na nchi za kikoloni, haswa Ufaransa, na katika miaka ya hivi karibuni jeshi la Ufaransa liliimarisha kuwepo kwake kijeshi katika nchi hizo kwa kisingizio cha kupambana na ugaidi. Hata hivyo, hali ya eneo hilo kama vile kuongezeka harakati za kigaidi na kuenea kwake barani Afrika, kulidhihirisha zaidi uzembe na kutoheshimu  nchi hizo  ahadi zao za kuboresha amani na usalama na kusaidia kuondoa athari za ukoloni barani humo.

Hali hiyo ilisababisha tawala za kijeshi ambazo zilitaka kuondoka askari jeshi wa kigeni kutoka nchi zao kupata uungaji mkono mkubwa wa wananchi. Pamoja na hayo, matukio ya  miezi ya hivi karibuni, yamesababisha kujiri mabadiliko makubwa zaidi ya kisiasa na kijamii katika eneo hilo la Afrika Magharibi.

Pamoja na hayo na katika miongo ya hivi karibuni, nchi za Afrika Magharibi zimejaribu kuboresha hali ya nchi za eneo hilo kwa kuimarisha ushirikiano wa kieneo na kuanzisha taasisi na asasi mbalimbali katika nyuga za kisiasa, kiuchumi na kiusalama. 

Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi ( ECOWAS ) ilianzishwa na nchi za Afrika Magharibi kwa nia na sababu hiyo, na nchi nyingi za eneo hilo ni wanachama wake.

Lakini jumuia hiyo ya kieneo imeshindwa kufikia malengo yaliyokusudiwa.  Hasa katika miaka ya hivi karibuni, na kufuatia mabadiliko ya kisiasa katika eneo hilo, ECOWAS  imekuwa ikiathiriwa na sera na matakwa ya nchi za kigeni, hasa Ufaransa, na katika baadhi ya migogoro ya kisiasa na kiuchumi imekuwa ikichukua maamuzi  kulingana na matakwa na ushawishi wa madola hayo ya kibeberu. Kwa mfano, wakati wa mapinduzi ya Niger, jumuiya hiyo ya ECOWAS  ilitangaza chini ya mashinikizo ya Ufaransa na Marekani, kuingilia kati kijeshi nchini humo ikiwa vikosi vya kijeshi vya Niger havitamrudisha madarakani Muhammad Bazoum aliyekuwa rais wa nchi hiyo. 

Katika nchi ya Mali pia, baada ya kujiri mabadiliko ya uongozi, ECOWAS  ilijaribu kuingilia kati kisiasa kwa kutangaza vikwazo dhidi ya nchi hiyo.

Bunge la ECOWAS

Kwa hakika, kwa kuimarika itibari  na ushawishi wa taasisi za kikanda katika bara hilo, nchi za kikoloni na kibeberu pia zilifanya njama kwa njia tofauti kujipenyeza kwenye taasisi hizo, jambo ambalo limegeuza malengo na shabaha za taasisi hizo na hivi sasa baadhi ya wanachama wanajitoa kwa madai hayo hayo ya kudhibitiwa jumuiya hiyo na madola ya kibeberu. 

Sheikh Abubakr Kamaldin, mmoja wa viongozi wa kidini wa Ghana anasema katika muktadha huo kwamba, viongozi wa nchi za Afrika wanapaswa kuzingatia masuala muhimu kama vile changamoto za kiusalama, utekaji nyara katika nchi za Afrika na matatizo ya kiuchumi ambayo yamekuwa yakiwakabili wananchi wa bara la hilo kwa miaka mingi badala ya kutumia nguvu na uwezo wao katika kukabiliana na masuala ya mapinduzi.

Kwa hakika, kisingizio cha kuwekeza nchi za nje katika taasisi za kieneo huko barani Afrika, kimesababisha nchi tatu za Niger, Mali na Burkina Faso kuondoka rasmi katika jumuia ya ECOWAS. Taarifa ya nchi hizi tatu imesema kuwa, ECOWAS imepuuza malengo yake makuu ya kuimarisha  uchumi, maisha ya kijamii na kuboresha ushirikiano wa kiutamaduni wa nchi wanachama, na sasa imekuwa ni chombo cha kukidhi matakwa ya  majeshi ya kigeni katika eneo hilo.

Hivi sasa, na kwa kuzingatia matukio ya hivi karibuni ya magharibi mwa Afrika, inaonekana kuwa nchi za ukanda huo zimedhamiria kikwelikweli kuwa huru na kutegemea ushirikiano wao wa kikanda badala ya kuwa tegemezi kwa madola ya kikoloni kama Ufaransa.

Tags