Makumi wahofiwa kufa maji baada ya boti 2 kugongana Kongo DR
(last modified Wed, 14 Feb 2024 11:15:46 GMT )
Feb 14, 2024 11:15 UTC
  • Makumi wahofiwa kufa maji baada ya boti 2 kugongana Kongo DR

Makumi ya watu wameripotiwa kupoteza maisha katika ajali mbaya ya boti iliyotokea magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Afisa wa serikali, Eliezer Ntambwe jana Jumanne aliliambia shirika la habari la Associated Press kuwa, ajali hiyo ilitokea katika Mto Congo, mashariki mwa Kinshasa, mji mkuu wa DRC.

Ntambwe amesema sababu ya ajali hiyo haijajulikana mpaka sasa, na kwamba makumi ya watu hawajulikani walipo kufuatia ajali hiyo. Mashuhuda na manusura wa ajali hiyo wanasema boti hizo zilikuwa zimebeba abiria na mizigo kupita kiasi.

Awali, Alexis Mampa, Chifu wa Manispaa ya Maluku alinukuliwa na vyombo vya habari akisema kuwa hakuna abiria yeyote aliyepoteza maisha kwenye ajali hiyo.

Usafiri wa majini ni maarufu DRC

Ajali mbaya za boti hutokea mara kwa mara katika mito na maziwa ya Kongo DR, ambapo boti mara nyingi vyomo hivyo vya usafiri wa majini hupakiwa kupita kiasi. Nchi hiyo ina barabara chache za lami katika eneo lake kubwa lenye misitu, na kusafiri kupitia mito na maziwa ni jambo la kawaida.

Januari mwaka huu, watu zaidi 50 waliripotiwa kufa maji baada ya boti yao iliyoundwa kwa mbao kupinduka katika ziwa moja nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Aidha Oktoba mwaka jana, watu zaidi 50 walikufa maji na 167 hakitoweka baada ya mashua waliyokuwa wakisafiria kupinduka kwenye Mto Congo, kaskazini magharibi mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. 

Tags