Askari kadhaa wa Afrika Kusini wauawa na kujeruhiwa Kongo DR
(last modified Fri, 16 Feb 2024 02:47:34 GMT )
Feb 16, 2024 02:47 UTC
  • Askari kadhaa wa Afrika Kusini wauawa na kujeruhiwa Kongo DR

Wanajeshi wawili wa Afrika Kusini wameuawa huku wengine watatu wakijeruhiwa katika shambulizi la bomu lililolenga kambi ya wanajeshi hao mashariki ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Taarifa iliyotolewa jana Alkhamisi na Jeshi la Taifa la Afrika Kusini (SANDF) imesema bomu hilo lililenga kambi ya askari wa nchi hiyo walioko mashariki ya DRC na kusababisha maafa hayo.

Ijapokuwa Jeshi la Afrika Kusini halijalihusisha na kundi lolote la waasi shambulio hilo la Jumatano ambalo linadai halikuwa limekusudiwa kulenga kambi hiyo, lakini maeneo mengi ya mashariki ya DRC yanadhibitiwa na kundi la M23.

Jumatatu iliyopita, Afrika Kusini ilitangaza habari ya kutuma wanajeshi wake 2,900 mashariki mwa Kongo DR. Nchi hiyo ilianza kutuma askari wake huko Goma, mashariki ya DRC Disemba mwaka uliopita chini ya mwavuli wa Jumuiya ya Maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika SADC. 

Waasi wa M23

Uganda, Kenya na Burundi zimeshiriki katika operesheni za kulinda amani nchini DRC, pamoja na wanajeshi kutoka Sudan Kusini, Afrika Kusini, Tanzania na Malawi.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ilialika kikosi hicho cha SADC baada ya kusema kuwa haijaridhishwa na wanajeshi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC ambao walitakiwa kupambana na waasi wa M23.

Eneo la mashariki mwa DRC limekumbwa na mizozo na mapigano kwa takriban miaka 30 sasa, kutokana na harakati za makundi ya waasi wenye kubeba silaha, ya ndani na nje ya nchi hiyo.