Wasomi wa Misri wazionya nchi za Afrika kuhusu njama za Israel
Wataalamu wa masuala ya kisiasa nchini Misri wamezionya nchi zilizoko katika Ukanda wa Mto Nile juu ya njama chafu za utawala haramu wa Israel katika eneo hilo.
Twariq Fahmy mtaalamu wa masuala ya kisiasa katika ulimwengu wa Kiarabu na mhadhiri wa elimu ya siasa katika Chuo Kikuu cha Cairo ameyasema hayo katika mahojiano na mtandao wa habari wa al-Youm el-Sabe wa nchini Misri na kusema kuwa, Misri pia itapata madhara juu ya natija ya safari ya Waziri Mkuu wa Utawala wa Kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahu katika nchi za Kiafrika. Fahmy amesema kuwa, hasa kwa kuzingatia kwamba wakati Netanyahu alipokuwa katika nchi hizo zilizopo kando kando ya Mto Nile alijitahidi kuonyesha sura ya utu na ubinadamu ya utawala wa Kizayuni huku akisisitizia uungaji mkono wa Tel Aviv kwa ajili ya kuzisaidia nchi hizo ili kufikia ustawi wake. Amefafanua kuwa, hii leo Israel imeweka mkataba wa akubaliano ya ujenzi wa mabwawa mawili mapya nchini Ethiopia na Uganda na kwamba hali hiyo inalenga kwenye siasa za maji ya mto Nile kuelekea mafuta ya nchi hizo. Kwa upande wake Said al-Lawandi, mtaalamu mwingine wa masuala ya kimataifa ameongea na mtandao huo wa habari al-Youm el-Sabe na kusema kuwa, safari ya Benjamin Netanyahu katika nchi za Ukanda wa Mto Nile, inatia wasiwasi mkubwa na kwamba, lengo lake ni kuiweka Misri chini ya mashinikizo. Kwa mujibu wa al-Lawandi, Israel inafanya njama za kuifanya Misri kuwa nchi yenye ukame. Naye Muhammad al-Arabi, mkuu wa mrengo wa mahusiano ya kigeni katika bunge la Misri amesema kuwa, udhaifu wa nchi za Kiarabu ndio ulioifanya Israel kuweza kuthubutu kupanua siasa zake chafu hata katika nchi za Kiafrika.