Polisi ya Somalia yaimarisha doria nchini humo
Duru za usalama nchini Somalia zimeeleza kuwa, jeshi la polisi la nchi hiyo limeimarisha doria katika maeneo ya kusini mwa nchi hiyo ya Pembe ya Afrika.
Taarifa iliyotolewa leo na duru za usalama nchini humo imearifu kuwa, hatua za usalama zimechukuliwa sambamba na kuanza kwa mafunzo ya kijeshi ya miezi mitatu yanayowahusisha askari wa Umoja wa Afrika mjini Kismayo, kusini mwa Somalia. Kwa mujibu wa ripoti hiyo, hatua ya pili ya mafunzo ya kijeshi ya miezi mitatu ya askari hao wa AU nchini Somalia itafanyika kati ya mwezi Julai hadi mwezi Oktoba mwaka huu. Mafunzo ya kijeshi yaliyotajwa yatapelekea kuwepo kwa vikosi vingi vya usalama sanjari na kuweka magari ya doria katika maeneo ambayo yamekombolewa kutoka mikononi mwa wanamgambo wa kundi la kigaidi na kitakfiri la ash-Shabab.
Wakati huo huo jeshi la Somalia limetangaza hali ya tahadhari mjini Mogadishu, mji mkuu wa Somalia kwa ajili ya kukabiliana na shambulizi tarajiwa kutokaka kwa wanachama wa genge hilo. Wanachama wa kundi la ash-Shabab wameshadidisha mashambulizi yao katika siku za hivi karibuni, hujuma ambazo zimesababisha mauaji ya watu wengi.