Kutangazwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa Rais nchini Venezuela
(last modified Sat, 09 Mar 2024 02:56:24 GMT )
Mar 09, 2024 02:56 UTC
  • Kutangazwa tarehe ya kufanyika uchaguzi wa Rais nchini Venezuela

Baada ya kuzingatia mapendekezo mbalimbali ya wabunge na makundi ya upinzani, hatimaye Baraza la Taifa la Uchaguzi la Venezuela limeitangaza Julai 28, 2024 ambayo ni siku ya kumbukumbu ya kuzaliwa Hugo Chávez, Rais wa zamani wa nchi hiyo kuwa siku ya kufanyika uchaguzi wa urais.

Suala la kufanyika uchaguzi wa rais nchini Venezuela sasa limekuwa kiini cha midahalo ya kisiasa nchini humo. Wapinzani wanaoungwa mkono na Marekani, ambao kwa miaka kadhaa sasa wamekuwa wakitumia nyenzo mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii kukishinikiza chama tawala cha Venezuela hivi sasa kwa mara nyingine tena wametumia mazingira ya kufanyika uchaguzi nchini humo kama kisingizio cha kufikia malengo yao.

Upinzani ulisusia na kutoshiriki katika uchaguzi uliopita wa urais ambapo Nicolas Maduro alishinda kwa kura nyingi. Mrengo wa upinzani ulidai kuwa, ushindi wa Maduro katika uchaguzi huo ulipatikana kwa njia za udanganyifu na kuchakachua matokeo, madai ambayo yalipingwa vikali na serikali ya Caracas.

Madai hayo yaliipa serikali ya Marekani kisingizio zaidi cha kuweka shinikizo zaidi dhidi ya serikali ya Caracas; kiasi kwamba Donald Trump, rais wa Marekani wakati huo, alifanya njama za kila upande za mapinduzi huko Venezuela, akaiwekea vikwazo vizito nchi hiyo ya Amerika ya Kusini na kumtambua kiongozi wa upinzani Juan Gua umri wa miaka 39 alishika wadhifa wa Uspika wa Bunge la Taifa la Venezuela. Katika mwaka huo huo, na baada ya kuanza tena muhula wa urais wa Nicolas Maduro, spika huyo wa bunge alijitangaza kuwa rais wa muda wa Venezuela.

Hugo Chavez, Rais wa zamani wa Venezuela

 

Hata hivyo njama zote hizo zilifeli na kugonga mwamba. Hatimaye mwaka jana, wapinzani wa serikali ya Venezuela walivunja serikali yao ya mpito iliyojitangaza na kumaliza uongozi wa Juan Guaidó, kibaraka na kipenzi cha Wamarekani.Sasa kwa mara nyingine tena, sambamba na njama zake za kuidhibiti Venezuela hususan rasilimali za nishati kama vile mafuta na gesi, Marekani imezungumzia suala la uchaguzi nchini Venezuela na kuwataka viongozi wa chama tawala kuitisha uchaguzi ambao utawashirikisha pia wapinzani wa serikali. Takwa hilo lilikubaliwa na serikali ya Venezuela kwa lengo la kuimarisha mshikamano wa ndani na kutatua tofauti za kisiasa.

Sanjari na chama tawala kuafiki hilo kulianza mazungumzo kati ya timu mbili za mazungumzo za serikali na upinzani kwa upatanishi wa Norway. Hatimaye timu za mazungumzo zilitiliana saini makubaliano mnamo Oktoba 17, ili kuinua kiwango cha haki za kisiasa na dhamana ya uchaguzi. Katika makubaliano haya, ambayo yalifikiwa kati ya serikali ya Venezuela na kundi la upinzani la "Unitary Platform" huko Barbados, iliamuliwa kuwa, wagombea wote na vyama vya siasa katika uchaguzi ujao watapewa vibali vya kushiriki uchaguzi. Kufuatia makubaliano hayo, Marekani ilipunguza vikwazo dhidi ya sekta ya mafuta ya Venezuela kwa muda wa miezi sita.

Juan Guaidó

 

Muda mfupi baada ya makubaliano hayo, uchaguzi wa ndani wa vyama vya upinzani ulifanyika na Maria Corina Machado akashinda kwa wingi wa kura miongoni mwa wapinzani.

Hata hivyo, kutokana na kuwa Machado alikuwa akikabiliwa na tuhuma za ufisadi, Mahakama Kuu ya Venezuela ilikataa kumuidhinisha kushiriki katika uchaguzi wa urais.

Uamuzi huu wa Caracas ulikabiliwa na jibu kali kutoka Washington, na serikali ya Marekani ikatangaza kwamba, itarejesha vikwazo dhidi ya Venezuela ikiwa Machado hataruhusiwa kugombea katika uchaguzi ujao.

Filihali, uingiliaji kati wa nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani katika masuala ya ndani ya Venezuela umeongezeka na kushika kasi. Kulingana na maafisa rasmi, wagombea wa uchaguzi wa rais wa Venezuela wana muda wa kujiandikisha hadi kufikia Machi 25. Kwa muktadha huo, Machado na wapinzani wa serikali ya Venezuela wana muda mchache wa kujadiliana na serikali ya Maduro kuhusiana na suala hili na kufikia mwafaka.

Tags