Burundi yakanusha vikali madai ya kuwatesa wapinzani
Serikali ya Burundi imesema kuwa, ripoti ya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Huma Rights Watch kwamba, serikali ya Bujumbura imekuwa ikiwatesa wapinzani haina ukweli wowote.
Serikali ya Burundi imesema kupitia wizara yake ya haki za binadamu kwamba, ripoti hiyo ni bandia na haiakisi ukweli wowote.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, katika ripoti yake hiyo Human Rights Watch imetumia majina ya mashahidi wasiojulikana hivyo haina nafasi ya kuchunguzwa.
Wakati serikali yua Burundi ikitoa msimamo wake huo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yameendelea kusisitiza juu ya kuweko ukiukwaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo.
Katika ripoti yake ya hivi karibuni, Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch lilisema kuwa, serikali ya Burundi imekuwa ikitumia vyombo vya usalama kuwatesa wapinzani wake.
Baada ya kuwahoji wahanga 40 wa mateso hayo, Human Rights Watch imetoa ripoti ikisema kuwa mateso hayo kimsingi hufanyika kwa malengo ya kisiasa.
Itakumbwa kuwa, Burundi ilikumbwa na mgogoro wa kisiasa kufuatia hatua ya chama tawala nchini humo CNDD-FDD kumuidhinisha Rais Pierre Nkurunziza wa nchi hiyo kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi uliopita.