Mar 27, 2024 07:39 UTC
  • Familia Kenya zaanza kukabidhiwa miili ya wahanga wa Shakahola

Serikali ya Kenya imeanza kukabidhi miili ya watu waliofariki dunia kutokana na njaa katika msitu wa Shakahola pwani ya nchi hiyo, baada ya kuagizwa na mchungaji mwenye misimamo ya kufurutu ada, Paul McKenzie kufunga hadi kufa ili eti wakakutane na Yesu (Nabi Isa AS).

Zoezi hilo la kukabidhi miili ya wahanga hao lilianza jana, ambapo miili saba ilikabididhiwa kwa família husika kwa ajili ya mazishi, takriban mwaka mmoja tangu kugunduliwa kwa makaburi ya umati kwenye msitu wa Shakahola, pwani ya Kenya.

Titus Ngonyo, mmoja wa watu waliopokea miili ya jamaa zao baada ya kupewa ushauri wa kisaikolojia na wanachama wa Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu amenukuliwa na shirika la habari la Anadolu akisema kuwa, "Moyo wangu una majonzi na simanzi tele kwa kupoteza watu wanne wa familia yangu. Naiomba serikali inisaidie katika mpango wa mazishi kwa kuwa sina pesa za kugharamia mazishi hayo."

Shakahola ni eneo la msitu linalopatikana huko Malindi katika Kaunti ya Kilifi, ambapo mhubiri tata wa Kikristo mwenye misimamo mikali, Kasisi Paul Nthenge Mackenzie alikuwa akiendesha shughuli zake pamoja na wafuasi wake.

Anasemekana aliwahimiza wafuasi wake kufunga kula na kunywa ili waage dunia eti waende kumuona Nabi Isa Masih AS (Yesu). Idadi kubwa ya wafuasi wa kanisa hilo walipoteza maisha kwa kufuata agizo hilo.

Mackenzie na wafuasi wake kadhaa wa Kanisa la Good News International walikamatwa mwaka jana mwezi Aprili na wamekuwa kizuizini tangu wakati huo ili kutoa nafasi kwa uchunguzi. 

Miili ya watu 429 wakiwemo watoto imefukuliwa kutoka maeneo ya makaburi huko Shakahola na uchunguzi umebaini kuwa mbali na kufa njaa wengine wakibainika kupoteza maisha kupitia kunyongwa. Mamlaka nchini Kenya zimelipiga marufuku kanisa hilo na kulitaja kuwa ni genge la uhalifu lililojipanga kitaasisi.

Mackenzie na viongozi wenzake wanakabiliwa na mashitaka ya mauaji, kuua bila kukusudia, kunyanyasa, kuwasababishia watu madhara mwilini, kujihusisha na uhalifu uliopangwa, kueneza itikadi kali, kufanikisha vitendo vya kigaidi na kadhalika.

Tags