Apr 16, 2024 10:47 UTC
  • Takriban watu 1,000 wapoteza makazi yao kutokana na mafuriko makubwa mkoani Arusha, Tanzania

Takriban watu 1,000 wameachwa bila makazi kutokana na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa inayoendelea kunyesha katika mkoa wa Arusha wa kaskazini mwa Tanzania.

Mkuu wa mkoa wa Arusha, Paul Makonda, amesema kukwa watu hao wameachwa bila makazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji au kuharibiwa na mafuriko katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Sehemu moja ya taarifa ya Makonda imesema: “Mamlaka za mkoa zimoa katika kukusanya hesabu ya hasara iliyosababishwa na mafuriko hayo kabla ya kutoa tathmini ya mwisho.” Amesema hayo baada ya kutembelea na kukagua maeneo yaliyoathiriwa na mafuriko mkoani humo.

Vilevile amewataka wananchi na wakazi wa maeneo yaliyokumbwa na mafuriko kuhamia maeneo ya juu ili kuepusha madhara zaidi.

Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Serikali ya Tanzania ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari, Mobhare Matinyi alisema Jumapili kuwa, watu 58 wamepoteza maisha kutokana na mafuriko katika mikoa 10 ya Tanzania Bara kwenye kipindi cha wiki mbili zilizopita wakiwemo 10 wa Mkoa wa Arusha.

Matinyi alitoa ripoti za polisi kwamba watu 58 walipoteza maisha kati ya Aprili 1 na 13 kutokana na mafuriko hayo ambayo yameathiri sehemu mbalimbali za Tanzania ikiwemo Rufiji.