Pande hasimu nchini Sudan Kusini zatangaza usitishaji vita
Pande mbili zinazohasimiana huko Sudan Kusini na kusababisha kuzuka upya kwa vurugu nchini humo zimetangaza kusitishwa kwa mapigano, baada ya kuwepo kwa siku kadhaa za machafuko mjini Juba zilizosababisha vifo vya mamia ya watu.
Baada ya Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini kutangaza usitishaji vita, masaa machache baadaye makamu wake Riek Machar naye ametoa amri kwa vikosi vyake vitiifu kusitisha mapigano.
Tangazo la usitishaji vita la pande mbili limeleta ahueni hasa baada ya kuzuka wasiwasi mkubwa nchini humo kufuatia mapigano yaliyoanza siku ya Ijumaa kati ya vikosi vya Rais na Makamu wa Rais katika mji mkuu Juba.
Mapigano baina ya majeshi yanayomtii Rais Salva Kiir na yale yanayoongozwa na Makamu wa Rais wa kwanza Riek Machar yametishia kuharibu mkataba wa amani uliosainiwa mwaka jana wa kumaliza miaka miwili ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mapigano yaliyozuka siku ya Ijumaa kati ya pande mbili ni ya kwanza kutokea tangu kuundwa serikali ya umoja wa kitaifa nchini humo.
Huko nyuma nchi hiyo changa zaidi barani Afrika iliwahi kutumbukia katika vita vya ndani baada ya Rais Salva Kiir kutoka kabila la Dinka kumtuhumu makamu wake wa zamani, Riek Machar wa kabila la Nuer kwamba alihusika na jaribio la kupindua serikali yake.