May 09, 2024 02:31 UTC
  • AU yailaani Israel kwa kupanua mashambulizi yake hadi Rafah

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amelaani vikali mashambulizi ya utawala haramu wa Israel katika mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Katika taarifa jana Jumatano, Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika amesema AU inakosoa vikali hatua ya Israel ya kupanua mashambulizi yake hadi katika kivuko cha Rafah.

Rafah ndicho kivuko kikuu cha kuingiza misaada ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza kwa ajili ya kuwasaidia watu madhulumu na wasio na ulinzi wa Palestina, wanaokandamizwa na utawala ghasibu wa Israeli.

Mahamat ameeleza bayana kuwa, "Matokeo ya vita vya Israel dhidi ya Gaza katika kila lahadha, ni mauaji ya kutisha na uharibifu mkubwa ulioratibiwa wa mali na miundomsingi."

Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU

Kadhalika Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU ametoa mwito kwa jamii ya kimataifa kushirikiana ili kukomesha ghasia na umwagaji damu huko Gaza, na kuleta amani ya kudumu katika eneo izima la Mashariki ya Kati (Asia Magharibi).  

Utawala wa Kizayuni wa Israel unaendelea kushambulia maeneo mbali mbali ya mashariki mwa mji wa Rafah, kusini mwa Ukanda wa Gaza tangu juzi Jumanne. 

Hadi sasa makumi ya Wapalestina wameuawa shahidi na wengine wengi kujeruhiwa katika mashambulizi hayo ya umwagaji damu ya utawala wa Kizayuni huko Rafah.

Tags