Waziri wa zamani wa Burundi katika EAC auawa Bujumbura
Waziri wa zamani wa Burundi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Hafsa Mossi ameuawa kwa kufyatuliwa risasi nje ya nyumba yake mjini Bujumbura.
Familia ya mwanadiplomasia huyo imesema marehemu ameuawa karibu na makazi yake mjini Bujumbura kwa kufyatuliwa risasi mbili na watu wasiojulikana.
Habari zinasema kuwa, Hafsa Mossi ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) ameuawa baada ya kushuka kwenye gari lake kwenda kutizama gari lenye vioo vyeusi lililokuwa limegonga gari lake kutoka nyuma. Hafsa Mossi ni ofisa wa serikali ya Bujumbura wa hivi punde kuuawa na genge la wabeba silaha lisilojulikana.
Mauaji haya yamefanyika katika hali ya ambayo, juhudi za kuupatia ufumbuzi mgogoro wa kisiasa katika nchi hiyo ya Kiafrika zimeendelea kukumbwa na vizingiti. Hii ni baada ya vyama vitano vya siasa kususia duru ya pili ya mazungumzo kati ya serikali ya Burundi na wapinzani huko Tanzania iliyoanza jana Jumanne na inatazamiwa kumalizika kesho. Vyama hivyo ambavyo ni FNL, FROLINA, PIEBU ABANYESHAKA, RADEBU na FRODEBU vimesusa kushiriki mazungumzo hayo ya amani kulalamikia hatua ya rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa, ambaye ndiye mwenyekiti wa mazungumzo hayo kuwajumuisha katika mazungumzo hayo Warundi wanaotuhumiwa kuhusika na ukiukaji wa haki za binadamu nchini, wakiwemo Pacifique Nininahazwe wa chama FOCODE, Armel Ningoyere wa chama cha ACT na mwanasiasa Minani Jean.
Duru ya kwanza ya mazungumzo ya kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa Burundi uliosababisha vifo vya watu zaidi ya 450 hadi sasa, ilifanyika huko huko Arusha chini ya upatanishi wa Benjamin Mkapa. Hata hivyo muungano mkuu wa upinzani Burundi haukualikwa katika mazungumzo hayo.