Kipindupindu chaua watu 123 Somalia, UN kuongeza juhudi za kukabiliana nacho
Katika taarifa yao ya pamoja, serikali ya Somalia na Shirika la Afya Duniani (WHO) zimesema kuwa, mwitiko wa kukabiliana na mripuko wa kipindupindu nchini Somalia bado ni mdogo huku idadi ya vifo ikiongezeka na kufikia watu 123 tangu mwezi Januari.
Ripoti ya pamoja ya pande hizo mbili imesema katika taarifa yao ya pamoja iliyotolewa Mogadishu, mji mkuu wa Somalia, kwamba, jumla ya kesi 14,389 za kipindupindu zilizoambatana na vifo vya makumi ya watu zimeripotiwa mwaka huu nchini humo.
Ripoti hiyo imeongeza kwamba, kulikuwa na upungufu mkubwa wa kesi za kipindupindu katika wiki ya pili ya mwezi huu wa Juni ikilinganishwa na kesi zilizoripotiwa katika wiki ya kwanza.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa kesi za ugonjwa wa kipindupindu zimeongezeka kote nchini Somalia, jambo ambalo linachangiwa na ufinyu wa upatikanaji wa maji safi ya kunywa na uchafuzi wa vyanzo vya maji vilivyoharibiwa na mafuriko, kiwango kikubwa cha utapiamlo miongoni mwa watoto, ukosefu wa huduma bora za vyoo, ugumu wa maisha na idadi ndogo ya vituo vya afya.
Kwa mujibu wa WHO, Somalia ina mripuko wa kipindupindu wa kuendelea ambao umezidi kuwa mbaya tangu yalipotokea mafuriko ya mwezi Disemba 2023, ambayo yaliharibu vyoo na kusababisha watu wengi kuhama makazi yao.
Mwaka 2023, zaidi ya kesi 18,304 za kipindupindu zilizosababisha vifo vya watu 46 ziliripotiwa nchini Somalia, huku zaidi ya nusu ya wagonjwa na wahanga wa ugonjwa huo wakiwa ni watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.