Polisi wa Kenya washutumiwa kwa kumuua mmoja wa waandamanaji Nairobi
Asasi za kiraia na mashirika ya kutetea haki za binadamu yameijia juu polisi ya Kenya kwa tuhuma za kumuua kwa kumpiga risasi mmoja wa waandamanaji wanaopinga mpango wa kuongeza ushuru, kodi na tozo.
Vyombo vya habari vimeripoti kuwa, mwanaharakati Rex Kanyike Masai, 29, aliaga dunia jana usiku kutokana na majeraha ya risasi, aliyopigwa akishiriki maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha wa 2024 katika barabara ya Moi jijini Nairobi.
Habari zaidi zinasema kuwa, Rex alipigwa risasi mguuni na maafisa wa polisi alipokuwa akishiriki maandamano hayo, na aliaga dunia akitibiwa katika hospitali jijini hapo.
Maandamano ya kupinga Muswada wa Fedha yameshika kasi jijini Nairobi na katika miji mingine mikubwa ya nchi hiyo, huku biashara nyingi zikisalia kufungwa.
Maelfu ya waandamanaji, wengi wao wakiwa ni vijana wa kizazi cha sasa (Gen Z) wamekuwa wakiandamana tokea Jumanne iliyopita, wakimkosoa Rais William Ruto na serikali yake kwa kuwatelekeza vijana kinyume na alivyoahidi katika kampeni zake na manifesto ya Kenya Kwanza.
Makundi ya kiraia yamewakosoa vikali maafisa usalama nchini Kenya hasa katika mji mkuu, Nairobi, kwa kutumia nguvu kupita kiasi kukabiliana na waandamanaji.
Amnesty International imesema kwa akali watu 200 walijeruhiwa jana jijini Nairobi, huku zaidi ya 100 wakikamatwa katika miji mbali mbali ya Kenya kwa kushiriki maandamano hayo.
Hii ni katika hali ambayo, Wabunge hapo jana walipitisha Muswada wa Fedha 2024 katika wasilisho lake la pili, licha ya pingamizi nyingi kutoka kwa umma. Baada ya upigaji kura uliofanyika jana alasiri, wabunge 204 walipiga kura ya ‘Ndio’ huku 115 wakipiga kura ya ‘Hapana’. Hii inamaanisha kwamba muswada huo umepita hatua ya pili na unaingia hatua ya tatu ambapo ukipita pia, utakuwa sheria.