Afrika yahimizwa kutumia mno teknolojia ya AI kuharakisha ustawi na maendeleo
Bara la Afrika limehimizwa kutumia fursa zinazopatikana kwenye teknolojia ya Akili Mnemba au Artificial Inteligence (AI) kwa kimombo ili kustawisha uchumi na kuongeza idadi na ufanisi kwa wafanyakazi wake.
Mwito huo umetolewa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Afrika chini la kaulimbiu ya "AI na Mustakabali wa Kazi barani Afrika," na kuongeza kuwa, teknolojia ya Akili Mnemba ya uzalishaji inatoa fursa na uwezo mkubwa wa kuwa na mustakabali wenye heshima wa kazi barani Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kushughulikiwa kikamilifu changamoto na kutumiwa vizuri fursa, kutaiwezesha Afrika kupata nguvu zaidi za kukuza na kustawisha uchumi wake, kuwezesha nguvu kazi yake ya vijana na kuongoza hata dunia katika maendeleo ya Akili Mnemba inayosaidia jamii.
Ripoti hiyo imeongeza kuwa, idadi ya vijana barani Afrika na mfumo uliochangamka wa ikolojia na teknolojia hiyo, ni fursa muhimu sana za kuweza bara hilo kuwa kiongozi duniani katika uvumbuzi wa kiteknolojia na maendeleo endelevu.
Wakala huo wa maendeleo ya bara la Afrika umetilia mkazo pia haja ya kuwekeza katika miundombinu ya kidijitali na mtaji wa watu, ikiwa ni pamoja na mipango ya elimu. Vile vile umesisitizia umuhimu mkubwa wa kuhakikisha kwamba maendeleo ya Akili Mnemba yanakuwa ni utatuzi wa changamoto nyingi barani Afrika.
Wakala huo pia umesema kuwa, kufikia mustakabali mzuri zaidi kutahitaji kuweko sera na kanuni zilizoundwa kwa uangalifu ambazo zitakuza maendeleo ya Akili Mnemba, kama ambavyo amehimiza pia kuanzishwa sera za kitaifa na kikanda za Akili Mnemba zitakazozingatia elimu-jumuishi, usalama wa wafanyikazi na kushikirishwa kikamilifu washikadau.