RSF yatangaza kuteka mji muhimu na wa kimkakati wa kusini mwa Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i113192-rsf_yatangaza_kuteka_mji_muhimu_na_wa_kimkakati_wa_kusini_mwa_sudan
Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kimetangaza kwamba kimeuteka kikamilifu mji muhimu na wa kimkakati wa el-Fula ambao ni makao makuu ya Jimbo la Kordofan Magharibi kutokana mikononi mwa jeshi la Sudan.
(last modified 2024-06-21T22:53:56+00:00 )
Jun 21, 2024 22:53 UTC
  • RSF yatangaza kuteka mji muhimu na wa kimkakati wa kusini mwa Sudan

Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) kimetangaza kwamba kimeuteka kikamilifu mji muhimu na wa kimkakati wa el-Fula ambao ni makao makuu ya Jimbo la Kordofan Magharibi kutokana mikononi mwa jeshi la Sudan.

Watu walioshuhudia wamesema kuwa, mapigano baina ya Jeshi la Sudan SAF na kundi la RSF yalianza Jumatano na baadaye vikosi vya RSF vimetangaza kuuteka kikamilifu mji huo. 

Mmoja wa watu hao alisema jana kwamba, mapigano hayo yalisimama Alkhamisi jioni baada ya RSF kuchukua udhibiti wa ngome ya jeshi na kusambaza vikosi vyake katika mji wote wa el-Fula ikiwa ni pamoja na kuteka maeneo yote ya serikali ya jimbo la Kordofan Magharibi, taasisi na soko kuu.

Mji wa el-Fula ni muhimu sana kutokana na kuwa na moja ya maeneo makubwa na muhimu zaidi ya mafuta nchini Sudan. Hata mabomba yanayosafirisha mafuta ya Sudan Kusini kupitia bandari ya Bashayer ya mashariki Sudan, pia yanapita katika mji huo wa el-Fula. Hadi wakati inaripotiwa habari hii, jeshi la Sudan lilikuwa bado halijatoa maelezo yoyote kuhusu madai hayo ya kundi la RSF.

Lakini serikali ya jimbo la Kordofan Magharibi imetoa taarifa na kulaani shambulio hilo la kundi la RSF na kusema kuwa wapiganaji wa kundi hilo wamefanya uporaji kwenye masoko na dhidi ya raia wasio na ulinzi na imetoa mwito kwa asasi za kiraia zinazopigana bega kwa bega na jeshi la Sudan kujiandaa kwa vita ili kuwatimua wanamgambo wa RSF.

Sudan imetumbukia kwenye vita vya uchu wa madaraka baina ya majenerali wa kijeshi tangu mwezi Aprili 2023 na vimeilemaza kikamilifu nchi hiyo.