Hali ya wakimbizi barani Afrika ni mbaya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i113200-hali_ya_wakimbizi_barani_afrika_ni_mbaya
Hali ya wakimbizi barani Afrika inaelezwa kuwa mbaya huku idadi ya wakimbizi ikiripotiwa kuongezeka kila siku katika mataifa mbalimbali ya bara hilo.
(last modified 2024-06-22T00:35:36+00:00 )
Jun 22, 2024 00:35 UTC
  • Hali ya wakimbizi barani Afrika ni mbaya

Hali ya wakimbizi barani Afrika inaelezwa kuwa mbaya huku idadi ya wakimbizi ikiripotiwa kuongezeka kila siku katika mataifa mbalimbali ya bara hilo.

Wakatii idadi ya wakimbizi ikiongezeka, ufadhili kwa ajili ya misaada kwa wakimbizi hao unazidi kupungua.

Mashirika ya misaada yanasema migogoro ya Sudan, Somalia, Sahel Afrika, na maeneo mengine yanapokea ufadhili mdogo, kuliko unaohitajika kushughulikia changamoto zinazowakabili.

Mapema mwezi huu, Mkuu wa Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC) amesema kutelekezwa kabisa kwa watu waliokimbia makazi yao limekuwa ni jambo la kawaida.

Taarifa ya Baraza la Wakimbizi la Norway (NRC) inasema, Burkina Faso ina zaidi ya watu milioni mbili waliokimbia makazi yao, na kuifanya kuwa moja ya janga la waliohamishwa lililopuuzwa zaidi duniani.

Wakimbizi wa Ukraine

 

Tarehe 20 Juni (jana) katika kalenda ya Umoja wa Mataifa, ni Siku ya Wakimbizi ulimwenguni. Siku hiyo huadhimishwa kila mwaka kwa njia mbalimbali.

Takwimu za Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) zinaonyesha kuwa, idadi ya wakimbizi duniani imefikia milioni 120.

Wanawake na watoto wadogo ndio wanaounda asilimia kubwa ya wakimbizi duniani. Watu hao ni wahanga wakuu wa udhalilishaji wa kijinsia, magendo ya binadamu, kufanywa watumwa, kutumiwa na magenge ya ya kigaidi na yenye silaha yanayofanya machafuko kwa maslahi yao binafsi. Umoja wa Mataifa unasema, wakimbizi hao wanahitajia mno misaada ya kifedha na kudhaminiwa usalama wao, kwani miongoni mwa sababu za kuwa wakimbizi ni matatizo ya fedha na kukosekana usalama hata wa chakula katika maeneo yao.