Jun 26, 2024 15:05 UTC
  • Rais William Ruto wa Kenya
    Rais William Ruto wa Kenya

Rais William Ruto wa Kenya amesema kwamba hatatia saini Muswada wa Fedha 2024 kuwa sheria. Ni baada ya maandamano makubwa ya siku kadhaa yaliyofuatiwa na mauaji ya waandamanaji mjini Nairobi jumanne ya jana.

Katika hotuba yake kwa taifa, Rais Ruto amesema mchana wa leo Jumatano kwamba, serikali imelazimika kuondoa Muswada wa Fedha wa mwaka wa 2024 na kwamba hatoutia saini kama ilivyotarajiwa.

Rais Ruto ameeleza kwamba, amewasikiliza kwa makini raia wa Kenya ambao wamesema kwa sauti kubwa kwamba hawataki chochote kuhusu muswada huo na kwamba amekubali yaliyosemwa na raia. 

"Baada ya kutafakari juu ya mazungumzo yanayoendelea kuhusu Muswada wa Fedha wa 2024 na kusikiliza kwa makini watu wa Kenya, ambao wamesema kwa sauti kubwa kwamba hawataki chochote kuhusiana na muswada huo, nakubali na kwa hivyo sitatia saini Muswada wa Fedha wa 2024 na utaondolewa baadaye. Wananchi wamezungumza.” Amesisitiza Rais Ruto.

Ruto amesema kwamba ataanza mazungumzo na vijana wa Kenya, bila kutoa maelezo zaidi.

Hatua hiyo imetajwa kuwa ushindi mkubwa kwa vijana ambao wamekuwa wakiandamana kwa wiki moja sasa wakipinga ongezeko la ushuru ambalo wanasisitiza litazidisha mzigo kwa wananchi na hali mbaya ya maisha inayowalemea Wakenya. 

Maandamano ya Wakenya kupinga Muswada wa Fedha 2024

Rais wa Kenya amesema serikali italazimika kuanza upya mchakato wa kutoa mapendekezo ya kukusanya fedha utakaohusisha wadau kutoka sekta mbalimbali.

Takriban watu 22 waliuawa katika maandamano ya jana Jumanne, kulingana na Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu ya Kenya (KNHRC) inayofadhiliwa na serikali.

Serikali ya Ruto inayokabiliwa na uhaba wa fedha ilikuwa imesema inalenga kuongeza ushuru ili kulipa deni kubwa la nchi la takriban shilingi trilioni 10 (Dola Bilioni 78), sawa na takriban asilimia 70 ya Pato la taifa la Kenya.

Tags