Rais wa Angola: Marais Kagame na Tshisekedi kukutana kwa mazungumzo
Rais Joao Lourenço wa Angola amesema kuwa, mazungumzo yanaendelea ili kuandaa "hivi karibuni" mkutano kati ya Marais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ili kufikia amani mashariki mwa DRC.
Rais wa Angola ambaye anahudumu kama msuluhishi aliyeteuliwa na Umoja wa Afrika (AU) amekuwa akifanya juhudi za kuwakutanisha viongozi hao wawili ingawa tarehe mahsusi ya kukutana ana kwa ana haijatangazwa hadi sasa.
Akizungumza nchini Ivory Coast katika ziara yake ya kikazi, Rais wa Angola amesema, tunafanya mazungumzo, katika ngazi ya mawaziri, tukiwa na matarajio ya hivi karibuni kuweza kuwaleta pamoja wakuu wawili wa nchi za DRC na Rwanda, kwa ajili ya mazungumzo ya moja kwa moja juu ya hitajio lisiloweza kuondolewa la kufikia amani ya uhakika.
Rais Felix Tshisekedi alisema hivi karibuni kwamba, yuko tayari kusitisha mpango wake wa kuanzisha vita na jirani yake Rwanda, ili kutoa nafasi kwa jitihada zinazoendelea za kupata suluhu ya mzozo unaoendelea mashariki mwa nchi hiyo.
Aidha Rais Kagame amewahi kunukuliwa akisema kwamba, siku zote amekuwa yuko tayari kukutana na mwenzake wa DRC kwa ajili ya mazungumzo na kwamba, hakuna wakati ambao aliweka masharti.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yanakanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.