Raia 6 wa China na askari 2 wa DRC wauawa mkoani Ituri
Waasi wa kundi la CODECO wameshambulia mgodi unaohusishwa na China katika jimbo lenye utajiri mkubwa wa dhahabu la Ituri, kaskazini mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuua raia sita wa China wa wanajeshi wawili wa Kongo.
Ruphin Mapela, Mratibu wa eneo la Djugu jana Alkhamisi alithibitisha habari ya kutokea shambulio hilo la umwagaji damu katika mgodi huo unaoaminika kumilikiwa na Wachina.
Naye mwakilishi wa shirika la Msalaba Mwekundu katika eneo la Djugu, Dhekana Ernest, amesema idadi ya wanajeshi wa DRC waliouawa katika hujuma hiyo ya waasi wa CODECO ni watatu, mbali na Wachina sita.
Wizara ya Mambo ya Nje ya China imetoa taarifa ya kulaani shambulio hilo la umwagaji damu katika eneo la Djugu mkoani Ituri. Imesema raia wengine kadhaa wa China hawajulikani walipo baada ya kutokea shambulio hilo.
Taarifa ya wizara hiyo imeitaka serikali ya DRC iwasake na kuwafikisha mbele ya sheria wahusika wa jinai hiyo haraka iwezekanavyo. Mao Ning, Msemaji wa Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya China amesema katika kikao na wanahabari mjini Beijing kuwa, "Tunafanya mawasiliano ya karibu na mamlaka za DRC kuhusu kuwatafuta raia wa China waliotoweka."
Kundi la wanamgambo la Ushirika wa Maendeleo ya Kongo (CODECO), moja kati ya makundi mengi yenye kujizatiti kwa silaha DRC, limekuwa likifanya mashambulizi ya umwagaji damu ya mara kwa mara nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, hasa mashariki mwa nchi hiyo.
Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Juni, watu 23 waliuawa katika mashambulizi ya waasi hao wa kundi la CODECO katika vijiji kadhaa kwenye jimbo lenye utajiri mkubwa wa dhahabu la Ituri kaskazini mashariki mwa DRC.