IGAD yataka Sudan Kusini iwekewe vikwazo vya silaha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i11437-igad_yataka_sudan_kusini_iwekewe_vikwazo_vya_silaha
Jumuiya ya Ushirikiano wa Kieneo ya Mashariki mwa Afrika IGAD imetoa mwito wa kuwekewa vikwazo vya silaha Sudan Kusini kwa shabaha ya kukomesha mapigano mapya yaliyozuka nchini humo hivi karibuni na kusababisha mauaji ya mamia ya watu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Jul 17, 2016 11:24 UTC
  • IGAD yataka Sudan Kusini iwekewe vikwazo vya silaha

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kieneo ya Mashariki mwa Afrika IGAD imetoa mwito wa kuwekewa vikwazo vya silaha Sudan Kusini kwa shabaha ya kukomesha mapigano mapya yaliyozuka nchini humo hivi karibuni na kusababisha mauaji ya mamia ya watu.

Mahboub Maalim, Mkurugenzi Mkuu wa jumuiya hiyo ya kieneo ameyasema hayo pambizoni mwa kongamano la Umoja wa Afrika linalofanyika huko Kigali, mji mkuu wa Rwanda na kuongeza kuwa, moja ya njia za kuupatia ufumbuzi wa kudumu mgogoro wa Sudan Kusini ni kuwekewa vikwazo vya silaha viongozi wa nchi hiyo changa zaidi barani Afrika na makamanda wa jeshi wanaovuruga mchakato wa amani. Amesema mbali na hatua hiyo, kuna haja ya kuimarishwa kikosi cha Umoja wa Mataifa cha Kulinda Amani nchini humo UNMISS. Amesema IGAD inaunga mkono pendekezo la wakuu wa majeshi ya nchi za Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan na Uganda la kutaka kutumwa wanajeshi wa nchi hizo kwenda kuimarisha kikosi cha UNMISS. Umoja wa Mataifa una jumla ya wanajeshi 13,500 wa kulinda amani huko Sudan Kusini na 300 miongoni mwao ni kutoka Ethiopia.

Zaidi ya watu 300 wameuawa katika mapigano yaliyotokea huko Sudan Kusini siku kadhaa zilizopita kati ya wafuasi wa Rais Salva Kiir wa nchi hiyo na wa wale wa Makamu wake, Riek Machar katika mji mkuu Juba. Aidha mamia ya maelfu ya watu wamelazimika kuyakimbia makazi yao huku wengine wakitoroka nchi kutokana na mapigano hayo.