Viongozi wa Nigeria wakiri asilimia 80 ya wananchi ni maskini
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Nigeria amekiri kuwa asilimia 80 ya wananchi wa nchi hiyo wanaishi katika ukata wa kuchupa mipaka.
Gazeti la Daily Post linalochapishwa mjini Lagos limemnukuu Yemi Osinbajo akisema hayo jana Jumapili mjini Kigali Rwanda anakoshiriki katika kikao cha 27 cha wakuu wa nchi wanachama wa Umoja wa Afrika AU. Amesema, watu milioni 110 wanaishi katika umaskini wa kupindukia nchini Nigeria idadi ambayo ni asilimia 80 ya wananchi wote wa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Nigeria amesema kuwa, nchi yake inahitajia dola bilioni 2.5 kuweza kumaliza kikamilifu ukata nchini humo na kuongeza kuwa, umaskini ndiyo changamoto kuu inayoikabili serikali ya hivi sasa ya nchi hiyo.
Amesema serikali ya nchi yake inafanya juhudi kubwa za kung'oa mizizi yote ya umaskini nchini humo.
Mwaka 2010 karibu thuluthi mbili ya wananchi wa nchi hiyo walikuwa wanaishi chini ya ukata wa kupindukia kiasi kwamba walikuwa wanahitajia misaada ya dharura ya chakula na maji safi ya kunywa.
Nigeria ina watu milioni 182 na laki mbili na inahesabiwa kuwa nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika. Aidha nchi hiyo ndiye mzalishaji mkuu wa mafuta barani Afrika.