UNICEF: HIV/UKIMWI, sababu kuu ya vifo vya vijana Afrika
(last modified Mon, 18 Jul 2016 07:48:48 GMT )
Jul 18, 2016 07:48 UTC
  • UNICEF: HIV/UKIMWI, sababu kuu ya vifo vya vijana Afrika

Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF umesema virusi vya HIV na ugonjwa hatari wa UKIMWI vingali sababu kuu ya vifo vya vijana barani Afrika.

Hayo yamesemwa na Anthony Lake, Mkuu wa UNICEF katika ufunguzi wa Kongamano la 21 la kimataifa la kupambana na maradhi ya UKIMWI, lililoanza hii leo nchini Afrika Kusini chini ya kaulimbiu 'Bado ni mapema kusherehekea ushindi' na 'Njia ndefu iko mbele yetu.' Ofisa huyo wa UNICEF amesema ugonjwa huo hatari umeendelea kuangamiza tabaka la vijana wenye umri wa kati ya miaka 10-19 barani Afrika, licha ya jitihada za kimataifa za kukabiliana nao. Asilimia 70 ya watu wanaoishi na ugonjwa huo duniani ni vijana kutoka eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara barani Afrika. Aidha UNICEF imebainisha kuwa, kwa kila vijana wanne walioambukizwa virusi vya HIV mwaka jana 2015, watatu kati yao ni vijana wa kike. Karibu wasomi elfu 18, madaktari, wanaharakati, watetezi wa haki za binadamu na wafadhili wanashiriki kongamano hilo linalofanyika mjini Durban, Afrika Kusini kwa ajili ya kutathmini maendeleo yaliyopatikana katika kupambana na virusi hivyo vya HIV ambavyo hadi sasa vimeshaua zaidi ya watu milioni 30 duniani. Hii ni katika hali ambayo, Chris Beyrer, mkuu wa taasisi ya kimataifa ya kupambana na virusi vya HIV, amesema kuwa hivi sasa kumepatikana matumaini ya kutibiwa kikamilifu ugonjwa hatari wa Ukimwi na kusisitiza kuwa, kuna hatua muhimu lazima zichukuliwe kwa ajili ya kufanikisha suala hilo.