Rais Tshisekedi amtuhumu mtangulizi wake kwa kuwaunga mkono waasi
(last modified Wed, 07 Aug 2024 11:20:54 GMT )
Aug 07, 2024 11:20 UTC
  • Rais Tshisekedi amtuhumu mtangulizi wake kwa kuwaunga mkono waasi

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amesema kuwa Rais wa zamani wa nchi hiyo Joseph Kabila ameanzisha mkakati wa kuunganisha makundi yenye silaha na vyama vya kisiasa nchini humo dhidi ya serikali yake.

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemtuhumu Rais wa zamani wa nchi hiyo Joseph Kabila kuwa anaunga mkono muungano wa makundi ya waasi yaliyowekewa vikwazo na Marekani.  

Tshisekedi ameeleza kuwa Joseph Kabila alisusia uchaguzi na sasa anaandaa uasi kwa sababu yeye ni AFC akimaanisha muungano kwa jina la Alliance Fleuve Congo. Hiyo ni harakati ya kisiasa na kijeshi iliyoasisiwa mwezi Disemba mwaka jana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa shabaha ya kuyaunganisha pamoja makundi yanayobeba silaha, vyama vya kisiasa na taasisi za kiraia dhidi ya serikali ya Kinshasa. 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ameeleza haya katika mahojiano aliyofanyiwa na radio moja binafsi ya nchini humo. Hata hivyo hakutoa ushahidi wowote wa kuthibitisha madai yake hayo. 

Rais wa zamani wa Kongo, Joseph Kabila 

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo amemtuhumu mtangulizi wake Joseph Kabila kufuatia Marekani mwezi uliopita kutangaza kuuwekea vikwazo muungao huo kwa jina la  AFC. 

Tags