Watu 16 wauawa katika makabiliano baina ya waasi, wanamgambo DRC
Mapigano kati ya waasi na wanamgambo wanaoiunga mkono serikali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo yamepelekea kuuawa wanakijiji 16.
Afisa wa serikali katika eneo hilo amesema, mapigano hayo ni katika msururu wa ukiukaji wa usitishaji vita wa hivi punde uliotangazwa karibuni kwa lengo la kunusuru maisha ya mamilioni ya watu waliokimbia makazi yao katika eneo hilo.
Tovuti ya habari ya Africa News imeandika habari hiyo na kueleza kuwa, wanakijiji hao waliuawa katika eneo la Rutshuru, jimbo la Kivu Kaskazini, wakati wa mapigano kati ya waasi wa M23 wanaodaiwa kuungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, na wapiganaji wa vuguvugu la vijana la Wazalendo, ambao mara nyingi hushirikiana na vikosi vya usalama vya Kongo.
Isaac Kibira, afisa wa serikali za mitaa katika eneo la Rutshuru amesema, "Waasi wa M23 walivamiwa na vijana wa kundi la Wazalendo na kwa bahati mbaya, raia saba waliuawa."
Kibira ameongeza kuwa, makabaliano mengine yaliyoshuhudiwa huko Rutshuru jana Alkhamisi yalisababisha gari kuchomwa moto, na kuua abiria tisa waliokuwemo ndani yake.
Mamlaka za eneo la Rutshuru zimeeleza bayana kuwa, hakuna hata mmoja wa wanakijiji waliouawa aliyehusika katika mapigano baina ya pande mbili hizo hasimu.
Eneo la mashariki mwa DRC kwa muda mrefu sasa limekuwa likitawaliwa na harakati za makundi 120 yenye silaha, yanayopigania madini ya dhahabu na rasilimali nyingine za eneo hilo, huku yakifanya mauaji ya halaiki.