Aug 21, 2024 11:52 UTC
  • Watu 100 wahofiwa kufa maji katika ajali ya boti Kongo DR

Watu zaidi ya 100 wametoweka baada ya boti iliyokuwa imewabeba kupinduka na kuzama magharibi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Boti hiyo iliyokuwa na watu 300, ilikuwa ikielekea mji wa Nioki kutoka Oshwe ilipozama katika eneo la Kutu katika Mto Lukenie katika mkoa wa Mai-Ndombe.

Jacques Nzenza Mongie, msimamizi wa eneo hilo, aliwaambia waandishi wa habari Jumanne kuwa boti hiyo iligonga shina la miti chini ya maji na kupinduka na kuongeza kuwa, miili 20, ikiwa ni pamoja na ile ya wanawake wanne, ilikuwa imeopolewa kufikia Jumanne jioni, na shughuli  ya kuwasaka watu kadhaa ambao hawajulikani waliko inaendelea.

Idadi kamili ya walionusurika ilikuwa bado haijajulikana mpaka tunaena mitamboni, lakini vyombo vya habari vya ndani vimeweka idadi ya waliookolewa kufikia jana jioni kuwa 43.

Nkoso Kevani Lebon, Gavana wa jimbo la Mai-Ndombe, ametoa mkono wa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao kwenye ajali hiyo, na kutangaza kuwa hatua kali zitachukuliwa ili kuzuia ajali za boti.

Ajali hiyo imetokea miezi miwili baada ya boti nyingine kuzama mwezi Juni na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 80 katika mto Kwa, magharibi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Ajali mbaya za boti hutokea mara kwa mara katika maji ya Kongo hususan kutokana na kuwa vyombo vingi vya majini hupakia watu kupita kiasi. Nchi hiyo ina barabara chache za lami katika eneo lake kubwa lenye misitu, na usafiri mkubwa ni wa majini.

Tags