Ujerumani yaondoa wanajeshi wake wa mwisho Niger baada ya kutimuliwa
(last modified Sat, 31 Aug 2024 10:59:27 GMT )
Aug 31, 2024 10:59 UTC
  • Ujerumani yaondoa wanajeshi wake wa mwisho Niger baada ya kutimuliwa

Ujerumani imeviondoa vikosi vyake vya kijeshi kutoka nchi ya Niger katika eneo lenye machafuko la Sahel barani Afrika.

Katika hafla iliyofanyika huko Niamey jana Ijumaa, wawakilishi kutoka Wizara za Ulinzi ya Niger na Ujerumani walitia saini makubaliano ya kukamilisha "kuondoa wanajeshi na zana za Ujerumani kutoka Niger."

Maafisa wa Niger na Ujerumani jana Ijumaa walisoma taarifa za pamoja kutangaza kukamilika kwa mchakato wa kuondoka wanajeshi wa nchi hiyo ya Ulaya nchini Niger.

"Kujiondoa huku hakuashirii mwisho wa ushirikiano wa kijeshi kati ya Niger na Ujerumani, kwa kweli pande hizo mbili zimejitolea kudumisha uhusiano wa kijeshi," walisema.

Jeshi la Ujerumani la Bundeswehr lilisema kuwa, limewaondoa wanajeshi na vifaa 60 vya mwisho kutoka Niger. Kwa muda wa miaka minane, wanajeshi wa Ujerumani walikuwa wakihudumu katika Kikosi cha Kudumisha Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Mali (MINUSMA).

Mapema mwezi huu wa Agosti, wanajeshi wa mwisho wa Marekani waliondoka nchini Niger, zaidi ya mwaka mmoja baada ya viongozi wa mapinduzi kuwataka kuondoka.

Serikali mpya ya Niger iliwatimua wanajeshi hao vamizi wa Magharibi baada ya kupinduliwa Rais wa Niger aliyekuwa kibaraka mkubwa wa nchi za Magharibi mwezi Julai mwaka jana.