Miili 26 yapatikana baada ya boti ya wahamiaji kupinduka Senegal
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116252-miili_26_yapatikana_baada_ya_boti_ya_wahamiaji_kupinduka_senegal
Idadi ya vifo kutokana na boti iliyokuwa imebeba wahamiaji iliyopinduka katika ufuo wa Senegal imeongezeka hadi 26 kufuatia kugunduliwa kwa miili 17 zaidi Jumanne.
(last modified 2024-09-11T22:58:19+00:00 )
Sep 11, 2024 08:54 UTC
  • Miili 26 yapatikana baada ya boti ya wahamiaji kupinduka Senegal

Idadi ya vifo kutokana na boti iliyokuwa imebeba wahamiaji iliyopinduka katika ufuo wa Senegal imeongezeka hadi 26 kufuatia kugunduliwa kwa miili 17 zaidi Jumanne.

Jeshi la Wanamaji la Senegal lilisema kwenye chapisho kwenye X kwamba Kamba boti hiyo ya mbao ilikuwa imebeba zaidi ya wahamiaji haramu 100 kutoka mji wa Senegal wa Mbour wakati ilipozama muda mfupi baada ya kungoa nanga siku ya Jumapili.

Pwani za Senegal hutumiwa mara kwa mara na wahamiaji wa Kiafrika wanaoelekea katika Visiwa vya Kanari vya Uhispania, ambavyo vinatumika kama moja ya maeneo makuu ya watu wanaojaribu kufika Ulaya.

Hivi karibuni Mtumbwi mmoja uliokuwa na wahamiaji haramu umepinduka katika fukwe za Mauritania, inayopakana na Senegal, na kusababisha vifo vya wahamiaji 89. Mtumbwi huo ulikuwa unaelekea barani Ulaya na watu walioshuhudia wanasema kuwa, ulikuwa na abiria 170.

Sasa hivi kuna ulinzi mkali katika Bahari ya Mediterania hivyo magenge ya kusafirisha binadamu kimagendo barani Afrika yameamua kutumia nchi za Bahari ya Atlantiki, hasa Senegal na Mauritania kusafirisha watu kuelekea barani Ulaya kwa tamaa chapwa ya kupata maisha bora. Njia hiyo ni hatari mno hasa kutokana na mikondo yake mikubwa na mawimbi makali.