Rais wa Senegal avunja bunge, aitisha uchaguzi wa mapema Novemba
Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye amelivunja bunge la nchi hiyo linaloongozwa na upinzani na kuitisha uchaguzi wa mapema ili kumaliza mvutano kati ya bunge na serikali.
Katika hotuba ya kitaifa, Faye amesema uchaguzi wa haraka utafanyika Novemba 17 mwaka huu. Hatua hiyo imekuja miezi sita baada ya Faye kuchaguliwa kuwa rais akiwa katika kambi ya upinzani.
Amesema bunge ambalo sasa linaongozwa na chama alichokiangusha katika uchaguzi limefanya iwe vigumu kwake kutekeleza "mabadiliko ya kimfumo" aliyoahidi wakati wa kampeni.
Faye ametoa wito kwa wapiga kura kuwachagua wagombea wa chama chake cha Wazalendo wa Senegal Kwa Ajili ya Kazi, Maadili na Udugu (PASTEF) ili aweze kua na mamlaka kamili ya kutawala.
Bunge lililomaliza muda wake, lililochaguliwa mnamo 2022, lilitawaliwa na wanachama wa muungano wa Rais wa zamani Macky Sall wa Benno Bokk Yakaar (Umoja Katika Matumaini).
Mvutano kati ya serikali na bunge ulishadidi hivi karibuni baada ya wabunge wa upinzani kufuta mjadala wa bajeti na kutishia kuwasilisha hoja ya kuikosoa serikali.
Wabunge wa upinzani wamekosoa hatua ya Faye kulivunja bunge na kudai kuwa amefanya hivyo kuepusha kuwasilishwa kwa hoja ya kuikemea.
Katika taarifa, kundi hilo lilidai kuwa Rais Faye na Waziri Mkuu Ousmane Sonko wa "wanatumia idara za serikali kufanikisha maslahi yao ya kisiasa."