Raia wa Marekani, Uingereza wahukumiwa kifo DRC kwa jaribio la mapinduzi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116350-raia_wa_marekani_uingereza_wahukumiwa_kifo_drc_kwa_jaribio_la_mapinduzi
Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siku ya Ijumaa iliwahukumu kifo watu 37 wakiwemo raia watatu wa Marekani kwa kuhusika katika jaribio la kuipindua serikali hiyo ya kati mwa Afrika  mapema mwaka huu.
(last modified 2024-09-14T04:00:37+00:00 )
Sep 14, 2024 04:00 UTC
  • Raia wa Marekani, Uingereza wahukumiwa kifo DRC kwa jaribio la mapinduzi

Mahakama ya kijeshi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) siku ya Ijumaa iliwahukumu kifo watu 37 wakiwemo raia watatu wa Marekani kwa kuhusika katika jaribio la kuipindua serikali hiyo ya kati mwa Afrika  mapema mwaka huu.

Watu hao wamepatikana na hatia ya kujihusisha na uhalifu, kutekeleza mashambulizi, ugaidi na pia kufadhili ugaidi.

Aidha mbali na Wamarekani, watu wengine watatu ambao ni raia wa Uingereza, Ubelgiji na Kanada pia ni miongoni mwa waliohukumiwa kunyongwa.

Kesi hiyo ilianza mwezi Julai na ilihusu mapinduzi yaliyofeli mwezi Mei yaliyoongozwa na Christian Malanga, ambaye alianzisha mashambulizi kwenye ikulu ya rais na pia makazi ya Vital Kamerhe, spika wa wa Bunge la nchi hiyo.

Malanga aliuawa kwa kupigwa risasi wakati akijaribu kukwepa kukamatwa mara tu baada ya kurusha mubashara jaribio hilo la mapinduzi kupitia mtandao wake wa kijamii.

Wote waliopatikana na hatia wana siku tano za kukata rufaa.

Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo aliapishwa kwa muhula wa pili mwezi Januari baada ya uchaguzi ambao ulikumbwa na utata.

Maeneo ya Afrika Magharibi na Kati yamekumbwa na mfululizo wa mapinduzi katika miaka ya karibuni.