Afrika Kusini: Tumedhamiria kuendelea na kesi yetu dhidi ya Israel ICJ
Afrika Kusini imetangaza kuwa, imedhamiria kuendelea na kesi yake katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ), ambapo inaishutumu Israel kwa kufanya "mauaji ya halaiki" katika Ukanda wa Gaza.
Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametangaza kuwa, nchi yake itawasilisha tena malalamiko yake mnamo mwezi Oktoba.
"Sisi ni tunajali maoni ya wengine," amesema Bw. Ramaphosa, alipoulizwa kuhusu hili wakati wa mkutano na waandishi wa habari, "tumedhamiria kusogeza faili letu mbele."
Rais huyo wa Afrika Kusini amebainisha kwamba, Pretoria itawasilisha mwezi Oktoba mjini Hague, makao makuu ya (ICJ), "mkataba" wa "mamia na mamia ya kurasa" kuunga mkono kesi yake. "Tunaendelea kusihi kwamba mauaji ya kimbari lazima yakome na kwamba lazima kuwe na usitishaji vita na vivyo hivyo lazima mateka.warejeshwe.

Hivi majuzi pia Ofisi ya Rais wa Afrika Kusini ilitangaza katika taarifa yake kwamba, itaendelea kufuatilia kesi ya mauaji ya halaiki ya utawala wa Kizayuni katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) hadi hukumu yake itakapotolewa.
Sehemu ya taarifa ya ofisi ya Rais wa Afrika Kusini ilieleza kuwa, kesi ya jinai za utawala ghasibu wa Israel itaendelea mpaka pale Mahakama ya Kimataifa ya Haki itakapotoa hukumu yake, na tunatumai kuwa utawala wa Israel utazingatia miongozo ya muda.
Tarehe 29 Disemba 2023, Afrika Kusini iliwasilisha malalamiko dhidi ya utawala wa Kizayuni kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kwa madai ya kukiuka Makubaliano ya Kuzuia Mauaji ya Kimbari, ambayo yalipitishwa mwaka 1948.