Wafungwa 300 Nigeria waliotoroka baada ya gereza kubomoka hawajulikani waliko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116444-wafungwa_300_nigeria_waliotoroka_baada_ya_gereza_kubomoka_hawajulikani_waliko
Wafungwa wapatao 300 waliotoroka katika gereza moja nchini Nigeria hadi sasa bado hawajulikani walipo.
(last modified 2024-09-16T23:33:32+00:00 )
Sep 16, 2024 23:33 UTC
  • Wafungwa 300 Nigeria waliotoroka baada ya gereza kubomoka hawajulikani waliko

Wafungwa wapatao 300 waliotoroka katika gereza moja nchini Nigeria hadi sasa bado hawajulikani walipo.

Serikali ya Nigeria inasema, wapatao 300 hawafahamiki waliko, baada ya kutoroka jela katika mji wa Maiduguri ulioshuhudia mafuriko makubwa na kuharibu miundo mbinu likiwemo gereza hilo.

Wafungwa hao walitoroka baada ya gereza kubomolewa na mafururiko. Juhudii za kuwasaka wafungwa hao zinaendelea ingawa hadi sasa hazijazaa matunda.

Hata hivyo, maafisa wa magereza wamesema kuwa, wafungwa saba wamerejea jela, baada ya kutoroka wiki iliyopita.

Hii ni mara ya kwanza kwa serikali ya Nigeria, kukiri kutoroka kwa wafungwa baada ya mafuriko makubwa yaliyosabibishwa na mvua kubwa ambayo imekuwa ikinyesha, kuangusha kuta za jela ambayo wafungwa hao walikkuwa wakitumikia vifungo vyao.

Athari za mafuriko jirani na gereza la Maiduguri lililobomolewa na mafuriko

 

Mafuriko hayo makubwa, yamesababisha maafa ya watu 30 katika mji huo unaopatikana katika jimbo la Borno, na kuwaacha maelfu bila makaazi baada ya nyumba zao kusombwa na maji.

Aidha, kuvunjika kwa kingo za Bwawa la Alau, kumesababisha wanyama wakali kama mamba na nyoka kusombwa na maji hadi katika makaazi ya watu, baada ya mafuriko kuharibu mbunga ya wanyama inayomilikiwa na serikali.

Rais Bola Tinubu, jana alitembelea mji wa Maiduguri kujionea kwa karibu madhara makubwa yaliyosababishwa na mafuriko hayo makubwa.