Machafuko ya kikabila yaua watu 30 Papua New-Guinea
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116446-machafuko_ya_kikabila_yaua_watu_30_papua_new_guinea
Watu wasiopungua 30 wanaaripotiwa kuuawa katika mapigano mapya ya kikabila yaliyoikumba Papua-New Guinea.
(last modified 2024-09-16T23:34:10+00:00 )
Sep 16, 2024 23:34 UTC
  • Machafuko ya kikabila yaua watu 30 Papua New-Guinea

Watu wasiopungua 30 wanaaripotiwa kuuawa katika mapigano mapya ya kikabila yaliyoikumba Papua-New Guinea.

Ripoti zinasema kuwa, makabiliano ya risasi baina ya mamia ya wapiganaji wa kikabila huko, Papua New Guinea yamesababisha vifo vya takriban watu 30.

Vikosi vya usalama nchini humo vimepewa mamlaka ya dharura kuchukua hatua ya kuzima machafuko hayo.

Polisi ya Papua New-Guinea imesema katika taariifa yake kkwamba, machafuko hayo kwa mara ya kwanza yalizuka mwezi Agosti baada ya wachimbaji madini wasiokuwa na kibali kumjeruhi mmiliki mmoja wa ardhi katika bonde la Porgera, eneo mojawapo ambako kuna utajiri mkubwa wa dhahabu.

Mazungumzo ya kutafuta amani yalishindikana na hali imegeuka kuwa machafuko mabaya ya kikabila,ambapo siku ya Jumapili watu 30 waliuwawa huku mamia ya wanawake na watoto wakiachwa bila makaazi baada ya majumba kutiwa moto.

 

Maafisa wawili pia ni miongoni mwa waliouwawa. Kamishna wa polisi David Manning amesema kuwa, nguvu itatumika kurudisha utulivu katika eneo hilo la milimani.

Mwezi Februari mwaka huu nchi hiyo ilishuhudia mapigano mengine kama hayo ya kikabila ambapo kwa akali watu 53 waliuawa.

Papua New Guinea ni taifa linaloendelea lenye watu milioni 10 wenye lugha 800 katika sehemu muhimu ya kimkakati ya Pasifiki ya Kusini.