Wanamgambo wa CODECO waua raia 10 mashariki mwa DRC
Raia kumi wameuawa katika shambulio la usiku wa manane Jumanne lililofanywa na wanamgambo wa CODECO kwenye kijiji kimoja Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mkoa wa Ituri.
Hayo yalidokezwa Jumanne na mkuu wa utawala wa eneo hilo na kiongozi mmoja wa mashirika ya kiraia.
CODECO ni muungano wa makundi kadhaa ya waasi na ni miongoni mwa makundi mengi ya wanamgambo wanaopigania ardhi na rasilimali katika eneo lenye utajiri wa madini la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wanamgambo wa CODECO wamekuwa wakishutumiwa siku za nyuma na Umoja wa Mataifa kwa mashambulizi dhidi ya jamii nyingine ikiwa ni pamoja na wafugaji wa kabila la Hema. Umoja wa Mataifa unasema baadhi ya mashambulizi yanayotekelezwa na CODECO yanaweza kujumuisha uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Kulingana na afisa mkuu wa utawala katika eneo husika, Jean Marie Mateso, na kiongozi wa mashirika ya kiraia Jules Tsuba, usiku wa manane, wapiganaji wa CODECO waliingia katika kijiji kilicho eneo la Djugu, ambapo kuna wakazi wengi wanaotoka katika jamii ya Hema, na kuua watu 10 katika kaya mbili,
Mateso amenukuliwa na Reuters akisema wanamgambo wa CODECO walikata vichwa vya baadhi ya wahasiriwa. Amesema kuna wasiwasi kuwa wanamgambo hao watashmbulia vijiji zaidi.