Asilimia 33 ya wagonjwa wa mpox Burundi ni watoto na vijana
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i116524-asilimia_33_ya_wagonjwa_wa_mpox_burundi_ni_watoto_na_vijana
Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Burundi linasema asilimia 33 ya wagonjwa wa homa ya nyani au mpox nchini humo ni watoto wa kwenda shule wenye umri wa kuanzia miaka 5 hadi 19, na hivyo kuwa changamoto mpya wakati familia zinajiandaa kwa mwaka mpya wa masomo.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Sep 19, 2024 01:13 UTC
  • Asilimia 33 ya wagonjwa wa mpox Burundi ni watoto na vijana

Shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia watoto, UNICEF nchini Burundi linasema asilimia 33 ya wagonjwa wa homa ya nyani au mpox nchini humo ni watoto wa kwenda shule wenye umri wa kuanzia miaka 5 hadi 19, na hivyo kuwa changamoto mpya wakati familia zinajiandaa kwa mwaka mpya wa masomo.

Mwakilishi wa UNICEF nchini Burundi France Bégin amesema ongezeko la maambulizi ya mpox miongoni mwa watoto nchini Burundi wakiwemo wenye umri wa chini ya miaka mitano linatia wasiwasi mkubwa na kuwalinda ndio kipaumbele chetu.

Tangu kuthibitishwa kwa mgonjwa wa kwanza wa mpox nchini Burundi tarehe 25 mwezi Julai mwaka huu, taifa hilo la Maziwa Makuu barani Afrika limethibitisha kuweko kwa wagonjwa 564 , ambapo asilimia  62.9 wana umri wa chini ya miaka 19. Hali kadhalika kuna washukiwa 1,576 wa ugonjwa huo ambao tayari shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ulimwenguni, WHO limeidhinisha chanjo yake.

UNICEF inasema kumekuwa na matukio 1,774 ya maonyo ya uwepo wa ugonjwa huo katika wilaya zote 34 za wilaya za kiafya za Burundi kati ya 49 nchini kote, ambako wilaya 3 katika mji mkuu Bujumbura ndio kitovu cha mlipuko.

Watoto na jamii zilizoko hatarini zaidi zimekuwa waathiriwa zaidi wa mpox katika nchi za kusini na mashariki mwa Afrika.

Zaidi ya watoto milioni 3 nchini Burundi wakitarajiwa kurejea shuleni katika mwaka mpya ulioanza tarehe 16 mwezi huu wa Septemba, UNICEF na serikali wanaongeza jitihada ili waweze kurejea salama shuleni.