Seneta wa Nigeria: Jinai za Israel Gaza, Lebanon zinaonyesha UN haina maana
(last modified Fri, 27 Sep 2024 03:05:21 GMT )
Sep 27, 2024 03:05 UTC
  • Seneta wa Nigeria: Jinai za Israel Gaza, Lebanon zinaonyesha UN haina maana

Mwanasiasa wa ngazi ya juu wa Nigeria amesema kuwa, mauaji ya kimbari ya Israel dhidi ya raia wa Palestina katika Ukanda wa Gaza na huko Beirut, mji mkuu wa Lebanon yameonyesha kushindwa kwa dunia kushughulikia suala la Palestina, na pia imeonyesha namna Umoja wa Mataifa ulivyo butu kwa kushindwa kukomesha ukatili na unyama wa Israel.

Katika mahojiano maalum na Iran Press mjini Abuja, Seneta Shehu Sani ambaye anawakilisha jimbo la Kaduna ya Kati katika Baraza la Juu la Bunge la Nigeria amesema: "Kinachoshuhudiwa Mashariki ya Kati hivi sasa sio tu kuhusu haki za binadamu, bali ni kuhusu ubinadamu."

Seneta Shehu Sani ambaye pia ni Rais wa Baraza la Haki za Kiraia la Nigeria (CRCN) ameeleza kuwa, "Hii ni mara ya kwanza katika historia ya dunia kwamba maafa ya aina hii yanayotekelezwa kwa njia ya mauaji ya watu wengi yamekuwa yakifanyika bila kupingwa na kutozuiliwa hasa na mataifa ambayo yanajinadi kuwa ndiyo yenye mamlaka na nguvu kuu za uhuru na demokrasia duniani. Mauaji ya watu wasio na hatia huko Gaza na sasa huko Lebanon ni maafa ambayo yataendelea kuwasumbua wanadamu wote."

Mwanasiasa huyo wa Nigeria amebainisha kuwa, "Tulichoona huko Beirut ni mfano wa wazi wa jinsi dunia imeshindwa kushughulikia matatizo ya Palestina na Israel. Pia imeonyesha ubutu, uzembe, na ubatili wa Umoja wa Mataifa." 

Seneta Shehu Sani wa Nigeria

Mwanaharakati huyo wa haki za binadamu ameeleza bayana kuwa, mauaji ya Wapalestina zaidi ya 40,000 yaliyofanywa na Israel huko Gaza hayana uwiano wowote na wala hayawezi kuhalalishika kwa njia yoyote ile.

Akijibu swali la mwandishi wa Iran Press kuhusu jinsi Umoja wa Afrika unavyoweza kusaidia kukomesha ukatili wa Israel dhidi ya jamii ya wanadamu, Seneta Shehu Sani ametoa mfano wa msimamo uliotolewa na serikali ya Nigeria siku ya Jumanne katika mkutano wa 79 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani, ambapo Makamu wa Rais Kashim Shetima alisema Nigeria inapinga mauaji ya Israel huko Gaza; na pia akaongeza kuwa Wapalestina wanastahili kuwa na makazi yao wenyewe kwenye maeneo ambayo tayari yanatambuliwa na Umoja wa Mataifa na sheria ya kimataifa ambayo inapuuzwa.