BRICS: Viongozi wa Afrika wataka mapinduzi katika taasisi za kimataifa
(last modified Thu, 24 Oct 2024 11:52:17 GMT )
Oct 24, 2024 11:52 UTC
  • BRICS: Viongozi wa Afrika wataka mapinduzi katika taasisi za kimataifa

Katika hotuba zao za jana Jumatano, viongozi wa Afrika wanaohudhuria mkutano wa kilele wa mataifa ya BRICS nchini Russia walijikita katika kutoa mwito kwa taasisi za kimataifa kulitendea haki bara la Afrika.

Waasisi wa kundi la BRICS kama jina lake linavyoonesha ni Brazil, Russia, India, China na Afrika Kusini. Kundi hilo limekaribisha wanachama wapya ambapo baadhi yake ni Iran, Misri, Ethiopia na Muungano wa Falme za Kiarabu.

Uturuki, Azerbaijan na Malaysia zimetuma rasmi maombi ya kuomba uanachama ndani ya kundi hilo huku msururu mwingine mkubwa wa nchi za dunia nao ukiwa kwenye foleni ya kuomba kuruhusiwa kuwa wanachama wa BRICS. 

Akihutubia mkutano huo wa kilele wa BRICS, Rais Abdel Fattah el Sisi wa Misri amesema: "Maendeleo ya kimataifa yanaonesha kuweko mapungufu ya mfumo wa sasa wa kimataifa na si katika masuala ya kisiasa na usalama tu, lakini pia mapungufu hayo yanashuhudiwa katika masuala ya kiuchumi na maendeleo." 

Rais Ramaphosa wa Afrika Kusini 

 

Kwa upande wake, Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini ametoa mwito wa kufanyika mageuzi ya kimsingi katika Shirika la Biashara Duniani na kurekebishwa sheria za biashara ili kuwezesha ustawi wa viwanda.

Naye Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed amependekeza kufanyika mageuzi ndani ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Amesema: "Kwa pamoja, tunaweza kuleta mageuzi ambayo yatashughulikia masuala ya mataifa yanayoendelea na kuhakikisha kuwa sauti zao zinasikika katika jukwaa hilo la kimataifa."

Mkutano huo wa kilele wa siku tatu ndio mkutano mkubwa zaidi wa viongozi wa dunia kufanyika nchini Russia katika miongo kadhaa na umefanyika wakati nchi za Magharibi zikijaribu kuitenga Moscow kutokana na vita vya Ukraine.